Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jonas Mkude na rekodi ya Michael Laudrup

Jonasmkude20 1692954340145 (1).jpeg Jonas Mkude

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo Jonas Mkude wa Yanga ameingia kwenye rekodi ya kiungo wa zamani wa Denmark, Michael Laudrup, ya kuchezea timu mbili hasimu na kupata ushindi wa mabao matano akiwa katika kila upande.

Mkude, zao la timu ya vijana ya Simba, alipandishwa timu ya wakubwa msimu wa 2011/12 kutokana na ushauri Patrice Mutesa Mafisango, kiungo Mkongomani aliyekuwa Simba kwa mkopo akitokea Azam FC.

Simba ilikuwa ikitafuta kiungo wa ukabaji kwa ajili ya kuimarisha timu na Mafisango akawaambia viongozi wasihangaike kutafuta mchezaji wa kumsajili kwani kuna kijana kwenye timu ya chini ya miaka 20 anao uwezo.

Ndipo akapandishwa msimu wa 2011/12 na kusaidia Simba kushinda ubingwa wa Ligi Kuu.

Zaidi ya hapo, alicheza kwenye mechi ya mwisho ya ligi msimu huo, Mei 6, 2012 katika Uwanja wa Mkapa ambapo Simba iliifunga Yanga mabao 5-0.

Novemba 5, 2023 Mkude akiwa amehamia Yanga, akacheza mechi ya watani dhidi ya Simba na timu yake kushinda 5-1.

Hii ni rekodi ambayo haijawahi kuwepo kwa wachezaji wote waliowahi kuchezea timu hizi kongwe zaidi hapa nchini.

Juni Mosi, 1968, Yanga iliifunga Simba wakati huo ikiitwa Sunderland, mabao matano kwa bila kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

Mchezo huo ndiyo ulikuwa wa kwanza kwa ligi kufanyika kwenye uwanja huo.

Hapo kabla mechi zote za ligi kwa Dar Es Salaam zilikuwa zikichezwa Uwanja wa Karume, wakati huo ulioitwa Ilala Stadium.

Yanga ilienda kwenye mchezo huo ilitoka kuhamia kwenye jengo lao jipya la ofisi za makao makuu pale kwenye makutano ya Mitaa ya Mafia na Swahili, Kariakoo.

Hii ilikuja baada ya kuishi kwenye ofisi za kupanga kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwake.

Hata hivyo, mchezo huu ulikuwa wa marudiano baada ya kuvunjika kwa mchezo uliofanyika Machi 30, 1968.

Mchezo huu ulivunjika dakika ya 20 baada ya Emmanuel Mbele ‘Dubwi’ wa Sunderland kumshambulia kwa makonde mazito mwamuzi wa mchezo huo, Jumanne Salum, na kushindwa kuendelea na mchezo.

Hadi wakati huo Sunderland ilikuwa tayari imeshafungwa 1-0.

Ndipo ukapangwa kurudiwa Juni Mosi, na ulipofanyika Sunderland wakafungwa 5-0.

Maulid Dilunga aliifungia Yanga mabao mawili ya kipindi cha kwanza na kufanya mchezo uende mapumziko kwa matokeo hayo.

Saleh Zimbwe aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awadh Gesan, alifunga mabao mawili (la tatu na la tano) na Kitwana Manara akafunga bao moja (la nne).

Takribani miaka 10 baadaye Simba ililipa kipigo hiki, na chenji ikabaki pale Julai 19, 1977 ilipoifunga Yanga mabao 6-0.

Kuna uongo mkubwa kuhusu mechi hii kwamba eti Yanga iliondokewa na wachezaji wake ndiyo maana ikafungwa.

Huu ni uongo mkubwa kwa sababu hii mechi ilikuja mwaka mmoja baada ya wachezaji wale kuondoka na hapo kati walishakutana na matokeo hayakuwa mabaya namna hiyo.

Januari 1976 Yanga iliwafukuza nyota wake kadhaa, wakiwemo Manara Brothers, Kitwana na Sunday, pamoja na Leodeger Tenga.

Yanga ikafanya usajili mpya na kushiriki ligi ya mwaka 1976, wakati huo ligi ikichezwa kwa kufuata kalenda ya kawaida, yaani kuanzia Januari hadi Desemba.

Mwaka 1976 ligi ilianzia ngazi ya wilaya na Yanga ikiwa Wilaya ya Ilala ilifika hadi fainali ya ligi ya wilaya, na kufungwa 2-1 na Simba, Machi 20, 1976.

Simba ikawa mabingwa wa wilaya, na Yanga kuwa wa pili.

Msimu ukaisha, ukaja msimu mpya wa 1977 na Yanga ikafanya tena usajili na kushiriki ligi.

Ndipo Julai 19, 1977 ikakutana na Simba na kufungwa 6-0, huku Abdallah Kibadeni akifunga mabao matatu yaani hat trick.

Hii inabaki kuwa hat trick ya pekee kwenye mechi ya watani tangu kuanza kwa Ligi ya Taifa, 1965.

Zaidi ya Kibadeni, mabao mengine ya Simba yalifungwa na Jumanne Hassan aliyefunga mawili na Seleman Jongo wa Yanga aliyejifunga.

Mei 6, 2012 Simba iliifunga tena Yanga mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa, sasa Uwanja wa Mkapa.

Hii ndiyo mechi aliyokuwepo Jonas Mkude. Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi, aliyefunga mawili, Juma Kaseja moja kwa penalti, Patrice Mafisango aliyefunga moja kwa penalti, na Felix Sunzu aliyefunga kwa penalti pia.

Katika mechi zote hizi, hakuna mchezaji aliyecheza huku na huku, zaidi ya Jonas Gerrard Mkude.

Hii inamfanya awe mchezaji wa kwanza kutoka dozi kote kote kwa watani wa jadi hapa nchini.

Hii inakuwa kama alivyofanya Michael Laudrup, nyota raia wa Denmark, aliyezichezea timu mbili hasimu za Hispania.

Mwaka 1994, Laudrup akiwa FC Barcelona, aliiongoza timu yake kushinda 5-0 dhidi ya Real Madrid dimbani Camp Nou.

Baada ya msimu huo akahamia Real Madrid na katika mechi yake ya kwanza, akaiongoza timu yake kulipa kisasi cha 5-0 dhidi ya Barcelona, dimbani Santiago Bernabeu.

Kwa kufanya hivyo Laudrup anakuwa mchezaji pekee kwenye historia ya El Clasico kushinda kwa mabao matano akiwa na timu zote mbili dhidi ya timu hizi hizo.

REKODI YA KIBADENI YANUSURIKA

Maxi Nzengeli wa Yanga amefanya kosa kama Emmanuel Okwi wa Simba mwaka 2012 la kuipoteza nafasi ya kuweka alama kwenye mechi ya watani.

Abdallah Seif Athuman, maarufu kama Kibadeni, ndiye mchezaji pekee kufunga mabao matatu kwenye mechi ya watani.

Mwaka 2012 wakati Simba inaifunga Yanga mabao 5-0, Emmanuel Okwi akiwa tayari ameshafunga mabao mawili, alisabaisha penalti tatu lakini hakupiga hata moja.

Angechagua kupiga penati moja tu na kufunga basi angekuwa ameifikia rekodi ya Kibadeni.

Mwaka huu tena, Maxi Nzengeli wa Yanga akiwa tayari amefunga mabao mawili, ikitokea penati kwa timu yake.

Kama angechagua kupiga penalti hii na kufunga, basi angekuwa ameifikia rekodi ya Kibadeni...lakini haikuwa hivyo.

Tena tofauti na Okwi, Yanga ndiyo ilihitaji zaidi hattrick hii ili kumaliza jinamizi la Kibadeni, lakini ndiyo hivyo tena.

Bahati kama hizi huwa haziji mara nyingi, kwa hiyo Yanga inaweza kusubiri tena miaka kadhaa hadi kuifikia rekodi ya Kibadeni.

MAJINA KUJIRUDIA

Mwaka 1968 wakati Yanga inaifunga Sunderland 5-0, walikuwa na mchezaji anayeitwa Zimbwe (Salehe).

Jina la Zimbwe limejirudia tena safari hii, lakini likiwa upande wa Simba, Mohamed Hussein Zimbwe.

Kama utaenda mbali zaidi utapona hata jina la Manara linajirudia...wakati ule alikuwa Kitwana Manara, safari ni Haji Manara japo yeye hakuwa ndani ya uwanja...lakini alikuwa Yanga.

Lakini yote kwa yote, rekodi ya JONAS MKUDE ni kubwa sana!

Katika mchezo wa juzi Jumapili dhidi ya Simba, Mkude hakuanza kikosi cha kwanza bali aliingia katika dakika 88, kuchukua nafasi ya Mudathiri Yahya na kuandika historia hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live