Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

John Nditi, Morogoro

87142377beb7a105dd22819a38c9709a John Nditi, Morogoro

Thu, 15 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kupata ajali ya gari kwenye barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.

Ajali hiyo ilitokea jana mchana Kihonda katika Manispaa ya Morogoro, na inadaiwa kuwa chanzo chake ni dereva wa bajaji ambaye alikatisha kwa mbele na hivyo kusabisha kutokea ajali hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare alithibitisha jana ajali hiyo, na alifika katika hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa kumjulia hali Profesa Kabudi akiwa amelazwa kwenye wodi ya daraja la kwanza.

Baada ya kutoka wodini kumjulia hali, Sanare alisema hali ya Profesa Kabudi inaendelea vizuri, na kwamba taarifa kamili kuhusu ajali hiyo itatolewa na Polisi baada ya kufanya uchunguzi wao.

“Najua mngetaka kusikia na hata kumsikia…ni kweli imetokea ajali njia ya kwenda Dodoma nje kidogo ya mji wa Morogoro ambayo imemhusisha Waziri Profesa Kabudi,” alisema Sanare.

“Mimi nilikuwa kwenye ziara kwenye Wilaya ya Kilosa na huenda na yeye alikuwa akija kwenye kuangalia jimbo lake la uchaguzi, sisi tukiwa mbele tumefika katika Tarafa ya Ulaya,”

Hata hivyo, alisema alipigiwa simu kuwa Profesa Kabudi amepata ajali na ilibidi akimbie kurudi lakini tayari walikuta ameshafikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa kupatiwa matibabu.

Profesa Kabudi ni Mbunge mteule wa Jimbo la Kilosa akiwa ni miongoni mwa wagombea nafasi ya ubunge katika majimbo 20 yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa wamepita bila kupingwa.

“Tunashukuru madaktari walimpatia matibabu na nilipata bahati na viongozi wenzangu kumwona na anaendelea vizuri...ni kweli anaendelea vizuri, tunamshukuru Mungu na madaktari wamemcheki hana tatizo kubwa sana, anahitaji kupumzika na baadaye tutaonana na madaktari watatushauri,” alisema mkuu wa mkoa.

Aliwatoa wasiwasi Watanzania na wananchi wa Wilaya ya Kilosa kuwa licha ya Profesa Kabudi kupata ajali, lakini jambo la kumshukuru Mungu kuwa anaendelea vizuri.

Mkuu wa mkoa wakati akimjulia hali aliambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge), Tixon Nzunda, Katibu Tawala wa Mkoa, Emmanuel Kalobero na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Rita Lyamuya hakuwa tayari kuzungumzia hali za majeruhi kutokana na kubanwa na usimamizi wa matibabu ya waziri huyo na majeruhi wengine waliokuwemo ndani ya gari.

Chanzo: habarileo.co.tz