Mshambuliaji wa Simba, Pa Jobe Omar tayari ana mabao yake mawili kwenye mechi tatu za kwanza kwenye mashindano mawili tofauti na ametumia mechi mbili kujua ubora wa mabeki wa timu pinzani kisha akawekea mkakati wa kuwamaliza.
Mechi tatu, alizocheza Jobe ni ule mchezo wa kwanza wa Kombe la Azam Shirikisho (ASFC), dhidi ya Tembo akifunga bao lake la kwanza kisha akafuata mechi mbili za ligi akifunga mechi moja dhidi ya Mashujaa huku jana alikuwa tena uwanjani wakati timu yake ikicheza dhidi ya Azam FC.
Akizungumza nasi, Jobe alisema kwenye mechi mbili za ligi amepata picha halisi ya mabeki wa timu pinzani na amegundua kuwa wanatumia nguvu nyingi wakati wakipambana kumzuia lakini hilo wala halimtishi.
Jobe raia wa Gambia, alisema kitu ambacho amekifurahia ni kwamba wakati wanakaba hivyo pia wanafanya makosa ambayo ndio anataka kuyatumia kuwaadhibu kwa kuwafunga.
"Ukabaji wao wanatumia nguvu nyingi kidogo lakini sio jambo gumu kwangu hata mimi nina nguvu pia kitu ambachp nimefurahia ni kwamba wanafanya makosa ambayo ndio nataka kuyatumia,"alisema Jobe.
"Nataka kuyatumia makosa yao kuifungia mabao mengi Simba, najua sio rahisi kutumia kila nafasi lakini nataka kuweka utulivu nifunge kwa kadiri ninavyoweza na muda ambao nitapewa kucheza.
Aidha Jobe, aliongeza kuwa utamu wa kikosi chao cha Simba ni kwamba kinaundwa na wachezaji wazoefu wanaojua kumpa mipira mshambuliaji wa kati.
Alisema viungo wa Simba na hata mabeki ni wabunifu kwenye kuchezesha timu hatua ambayo kwao washambuliaji ni kitu muhimu ili waweze kufunga.
"Unaweza kuona kwenye timu yetu, hawa wote ni wachezaji wazoefu, akili yao ikiwa uwanjani inafanya maamuzi makubwa, kwa viungo na hata mabeki kama hawa ni kitu kizuri kwa washambuliaji ili tufunge zaidi."