UONGOZI wa Yanga umefunguka kuwa kuna uwezekano mkubwa wakaingia sokoni na kusajili beki mmoja wa kati mwenye uwezo mkubwa ili kuwa msaada kwa Dickson Job na Bakari Mwamnyeto ambao ndiyo tegemeo kwa sasa.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabiti Kandoro alipokuwa anaweka wazi mipango ya timu hiyo kwenye dirisha dogo la usajili ambalo limefunguliwa Desemba 16, mwaka huu na kutarajiwa kufungwa Januari 15, mwakani.
Kandoro alisema viongozi wametazama kikosi na kupitia ripoti ya mwalimu, wamegundua ili kudumu kwenye ubora walionao sasa ni vema wakasajili beki mmoja wa kati.
“Tunahitaji kuwa na timu iliyotimia kwenye kila idara, ukitazama kwa umakini utagundua Yanga inahitaji kuwa na beki mwingine wa kati, kariba ya kina Mwamnyeto na Job.
“Lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo mzito wale wachezaji, hiyo itasaidia timu kuwa na ubora ule ule ambao sisi tunahitaji kuona kwenye kila mechi,” alisema.