Dickson Job juzi usiku alifunga bao la kwanza la Ligi Kuu Bara tangu ajiunge na Yanga, huku akimtamba amemlipa Kibwana Shomaty anayecheza naye klabuni hapo ambao ni kama wana ligi yao na kupeana sasa mtihani kwa mechi nane zilizobakia kumaliza msimu huu.
Job alifunga bao moja kwenye ushindi wa 2-0 iliyoupata Yanga dhidi ya Namungo Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti mabeki hao ambao kila mmoja ametupia bao moja kwenye michezo 22 waliyocheza, walisema mchezaji kwa sasa wanachuana ili kupatikana wakutupia bao la pili kwenye mechi nane zilizobaki ndiye atakayekuwa mwalimu wa mwenzake.
Kibwana alisema mara baada ya Job kutupia juzi alimfunga mdomo, lakini anaamini yeye ndiye chachu ya ubora aliouonyesha na kufanikiwa kutupia anamuahidi kuwa akifunga kwenye mechi zilizobaki basi ndiye atakayekuwa mwalimu.
“Nafurahi amefunga na amenipa maneno mengi kuwa hiyo ndio kazi yake lilikuwa ni suala la muda tu, huku akijitamba eti amefunga bao bora katikati ya wachezaji wanaoitwa warefu kwake,” alisema Kibwana waliocheza wote Mtibwa Sugar na timu ya taifa ya Vijana kuanzia ile ya U17 na U20 na kuongeza;
“Nimekubali lakini tumekubaliana kuwa kwenye mechi nane zilizobaki mchezaji ambaye atapata nafasi ya kufunga ndiye atakuwa mwalimu wa mwenzake kwa sababu kila mmoja katupia bao moja moja hakuna mbabe.”
Job alisema alikuwa anaisubiri kwa hamu siku kama ya juzi kuhakikisha anasawazisha kile alichokifanya Kibwana kutokana na kumnyima raha baada ya kutupia sasa ni 50-50 wamepeana mtihani mwingine.
“Hakuna siku nilikuwa na raha kama jana (juzi) nilimnyamazisha kabisa Kibwana hakuwa na neno la kusema, pia nafurahi kuwa ndugu yangu ananipa changamoto ya kuhakikisha tunafanya vizuri kuipambania timu,” alisema Job anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars na kuongeza;
“Baada ya kutupia kazi iliyobaki ni kuhakikisha kwenye mechi nane zilizobaki pamoja na kuipambania timu isiruhusu bao hadi msimu unaisha ni kufunga na natamani kuwa wa kwanza ili niweze kuendelea kumpa somo kijana wangu namna ya kufunga.”