Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi Tchakei anavyopindua ufalme wa Bruno Singida

Marouf Tchakei Marouf Tchakei

Sun, 29 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unaweza kusema usajili wa kiungo mshambuliaji wa Singida Big Stars, Marouf Tchakei umelipa kwa kiasi fulani baada ya kuonyesha kiwango bora katika mashindano ya msimu huu.

Tchakei alijiunga na Singida msimu huu akitokea AS Vita Club na ameanza kuiteka nafasi ya kiungo mwenzake Bruno Gomez ambaye alikuwa kwenye kiwango bora msimu uliopita na kuwa gumzo katika Ligi Kuu Bara.

Kupitia gazeti hili tunakuletea jinsi Tchakei anavyopindua ufalme wa Mbrazili huyo taratibu katika kikosi hicho.

MSIMU ULIOPITA

Msimu uliopita katika kikosi cha Singida Big Stars eneo la kiungo lilikuwa ni kama mali ya Bruno pekee ambaye alikuwa tishio kwa timu pinzani. Viungo wengine katika kikosi hicho walikuwa wakibadilishana mara kwa mara.

Katika ligi hiyo Bruno alikuwa kwenye orodha ya wafungaji bora watano akiwa na mabao 10 sawa na Moses Phiri wa Simba na Aziz KI wa Yanga.

Nyota huyo alifanya vizuri na kuchaguliwa kuwania tuzo za Ligi Kuu Bara katika vipengele viwili, kile cha kiungo bora wa msimu ambapo tuzo hiyo ilichukuliwa na Saido Ntibazonkiza wa Simba na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka iliyoondoka na Fiston Mayele.

Msimu huu mpaka raundi ya sita Bruno hajafunga bao lolote wala kutoa asisti kama ilivyo msimu uliopita ambao alikuwa hatari na ni wazi ana kazi ya ziada msimu huu.

Kwa sasa kuna kiungo Morice Chukwu na Tchakei ambao wanaonekana kuwa hatari zaidi kwa timu za Ligi Kuu wakikipiga Singida Big Stars.

NI VITA

Hakuna anayebisha juu ya uwezo wa Tchakei na namna anavyoonyesha kiwango bora tangu atue Singida.

Kwa sasa katika kikosi hicho kuna vita ya viungo wawili, Bruno na Tchakei kama ilivyo kwa Yanga waliko kina Aziz KI na Pacome Zouzoua. Kutokana na kiwango anachoonyesha Tchakei, raia wa Togo ni wazi kwamba Bruno ana kazi ya ziada ya kurudi kama zamani.

Tchakei ambaye ni kiungo mshambuliaji anamudu pia kucheza kama winga na sifa zake hazitofautiani sana na Bruno wa msimu uliopita.

Pia ni mzuri kwenye mipira ya faulo na katika mabao sita aliyofunga msimu huu kwenye mashindano - mawili kafunga kwa penalti, shuti mawili na faulo mawili.

AACHIWA MSALA

Sasa kutokana na namna Tchakei anavyofanya vizuri ameachiwa msala wa kupiga mipira ya penati, faulo na friikiki peke yake.

Sio tu kwenye mechi mpaka mazoezini kiungo huyo kazi yake kubwa ni kupiga mipira hiyo na amekuwa akiitendea haki.

KIMATAIFA YUMO

Mchezaji huyo amefanya vizuri pia kwenye michuano ya kimataifa baada ya kufunga mabao matatu kwenye mechi nne za Kombe la Shirikisho. Kama kawaida yake alifunga penalti mbili dhidi ya JKU, timu yake ilipoondoka na ushindi wa mabao 4-1 mchezo wa kwanza.

Alifunga pia bao moja la kufutia machozi timu hiyo ilipotolewa katika makundi kwa jumla ya mabao 4-2 kwenye mechi ya mkondo wa pili ugenini dhidi ya Future FC ya Misri alipomalizia kwa kichwa shuti lililopigwa na mchezaji mwenzake, Duke Abuya. Msimu huu timu nne zilishiriki michuano ya kimataifa, Simba na Yanga (Ligi ya Mabingwa Afrika) huku Singida na Azam ikishiriki Kombe la Shirikisho.

Timu mbili za Tanzania ndizo zimesalia baada ya Singida na Azam kutolewa katika hatua za awali ambapo Simba iko Kundi B na Wydad AC (Morocco), ASEC Mimosas(Ivory Coast) na Jwaneng Galaxy ya Botswana huku Yanga ikiwa kundi D na timu za Al Ahly (Misri), CR Belouzdad (Algeria) na Mediama (Ghana).

LIGI KUU SASA

Kwenye Ligi Kuu Bara nako Tchakei hayupo nyuma kwani mpaka sasa amefunga mabao matatu kwenye mechi sita, ambapo alifunga mawili peke yake kwenye ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo.

Pia alifunga bao moja kwa shuti kali lililomshinda kipa kwenye mechi dhidi ya Azam FC ambapo timu hiyo ilipoteza kwa mabao 2-1.

Chanzo: Mwanaspoti