Jimmy Floyd Hasselbaink amejiuzulu kama kocha wa Burton Albion, ambao wako mkiani mwa League One.
Mholanzi huyo mwenye miaka 50, anaondoka wiki mbili tu baada ya kusema kwamba angeng'atuka ikiwa atajiona kama yeye ni tatizo kwenye klabu hiyo.
Mchezo wa mwisho kwa Jimmy kuinoa klabu hiyo alikula kipigo kutoka kwa Oxford, ambacho kinawafanya wabaki na pointi moja pekee kati ya mechi saba za kwanza msimu huu.
Meneja msaidizi Dino Maamria atachukua nafasi na kuwa kocha wa muda wa Burton.
Jimmy aliiongoza Burton kuwa mabingwa wa Ligi daraja la Pili mwaka wa 2015 wakati wa kipindi chake cha kwanza kama kocha kwenye Uwanja wa Pirelli.
Alirejea Januari 2021 wakati Albion walipokuwa mkiani mwa “League one” na kuwaongoza kumaliza katika nafasi ya 16.
Kabla ya kuanza kwa msimu huu, Hasselbaink alisema kikosi chake bado kinahitaji kujengwa.
Ukosefu wa rasilimali za kuimarisha kwa kiasi kikubwa tangu wakati huo hatimaye umesababisha kuondoka kwake.
“Nimeipeleka klabu kadiri niwezavyo na rasilimali chache zilizopo na ni wakati wa mtu mwingine kuingia na kuingiza nguvu mpya,” Jimmy aliambia tovuti ya Burton.