Siku chache baada ya Shakhtar Donetsk kutangaza wachezaji 33 ambao wamesajiliwa kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku Novatus Dismas akiwa mmoja kati yao, Anthony Kavunde ambaye anaishi nchini humo amechambua nafasi yake na kueleza juu ya bahati ya namba aliyopewa Mtanzania huyo.
Shakhtar ambao wanafahamika kwa jina la utani la Wachimbaji madini, imepangwa kundi H sambamba na bingwa mara tano wa michuano hiyo, FC Barcelona (Hispania), FC Porto (Ureno) na Antwerp ya Ubelgiji.
Kwa mujibu wa orodha hiyo yenye wachezaji 33, Novatus ambaye ni usajili mpya akitokea Zulte Waregem ya Ubelgiji amepewa jezi namba 25 ambayo awali ilikuwa ikivaliwa na kiungo, Georgiy Sudakov aliyeamua kubadilisha jezi yake na kuchukua namba 10 baada ya Mykhailo Mudryk kujiunga na Chelsea.
Anthony alisema, “Nimeona Novatus anaweza kucheza nafasi zaidi ya moja hiyo ni faida kwenye timu kwa sababu ni wachezaji wachache wenye uwezo wa kufanya hivyo, anaonekana ni mchezaji mwenye nidhamu na kujituma naamini atakuwa na wakati mzuri hapa, jezi namba 25 ni yenye bahati.”
Anaendelea kwa kusema, wapo wachezaji wengi ambao amewashuhudia wakivaa jezi namba 25 na kufanya vizuri akiwemo Sudakov msimu wa 2021/22.
“Nakumbuka kuna kipa alikuwa anaitwa Obolon-Brovar Kyiv alikuwa akifanya vizuri huku akiwa na jezi namba 25, wapo wachezaji wengi ambao wamefanya vizuri ila kwa hivi karibuni ni Sudakov,” alisema.