Juzi wakati wa hafla ya harambee ya kuzichangia timu za Taifa, ulifanyika mnada wa jezi zenye majina ya wachezaji wa zamani wa Taifa Stars huku jezi ya Kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa, Juma Pondamali 'Mwnsah' ikiuzwa bei kubwa kuliko zote.
Jezi hiyo iliuzwa Sh25 milioni akizipiku jezi nyingine tano zilizouzwa ukumbini hapo ikiwemo ya Agustino Peter 'Tino' aliyeifungia bao Stars kufuzu fainali za Afcon mwaka 1980 ambayo iliuzwa Sh7 milioni.
Jezi ya mchezaji Rashid Idd Chama iliuzwa Sh6.2 milioni ikifuatiwa na jezi ya Leodger Tenga iliyouzwa Sh6 milioni wakati jezi ya Juma Mkambi ikiuzwa Sh2.2 milion.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alisema mnada wa jezi zingine za wachezaji hao wakongwe zitauzwa kwa njia ya mtandao.
Akizungumza mara baada ya mauzo ya jezi yake, Pondamali amesema; "Ni fahari kubwa sana kwangu jezi yangu kupewa thamani kubwa na wadau wa soka, hiyo inaonyesha ni kiasi gani tulilitumikia taifa vyema na wadau bado wanakumbuka mchango wetu.
"Ni kitu kizuri kimefanyika kutuenzi kwa njia hii, tunaamini vijana wetu huko walikoenda pia watajitoa kuhakikisha wanafanya vyema kwenye fainali hizi za Afcon."
Katika hafla hiyo, Sh 3.7 Bilioni zilipatikana kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo ambapo lengo ni kupata Sh 20 Bilioni kwa ajili ya timu za Taifa zote zinazoshiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Na katika mipango ya muda mfupo ambayo imepangwa na Kamati ya kuhamasisha timu hizo ambayo ni mipango ya miezi mitatu imepanga kukusanya Sh 10 Bilioni.