Strika matata wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Novemba, wakati Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo wa Ligi Kuu ya NBC.
Kikao cha Kamati ya Tuzo za TFF kilichokutana mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, kilimchagua Jeremiah Juma baada ya kuonesha kiwango kizuri kwa mwezi Novemba akifunga mabao manne kwa timu yake, huku mabao matatu ‘hat trick’ akiyafunga katika mchezo dhidi ya Namungo ambao timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, hiyo ikiwa ni hat trick ya kwanza msimu huu wa Ligi.
Mshambuliaji huyo alisaidia timu yake kupata matokeo ikishinda michezo miwili na kutoka sare mmoja na kupanda kwenye msimamo kutoka nafasi ya 16 hadi ya nane katika msimamo wa Ligi hiyo yenye timu 16. Juma katika hatua ya fainali aliwashinda Meddie Kagere wa Simba na kipa wa Coastal Union, Mussa Mbissa.
Kwa upande wa Mayanga aliwashinda Pablo Franco wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga alioingia nao fainali, ambapo kwa mwezi huo Prisons ilionesha kiwango kizuri ikitoka mkiani mwa msimamo wa ligi hadi nafasi ya nane.