Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jentrix wa Simba Queens na rekodi za kibabe Ligi Kuu

Jentrixxxxxxx Jentrix wa Simba Queens na rekodi za kibabe Ligi Kuu

Thu, 27 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Moja ya majina yanayotamba kwa sasa kwenye Ligi Kuu ya Wanawake nchini (WPL) ni Jentrix Shikangwa ambaye amekuwa tishio kwa makipa akiwatungua anavyotaka na kutangaza ufalme kwenye mbio za ufungaji bora.

Mshambuliaji huyo wa Simba Queens raia wa Kenya akitumia zaidi mguu wa kushoto alijiunga na timu hiyo dirisha kubwa na kutambulishwa Septemba 27, 2022 akitokea Fatih Karagumruk SK ya Uturuki, baada ya mkataba wake wa muda mrefu na timu hiyo kusitishwa ghafla.

Alicheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Wekundu wa Msimbazi, Oktoba 11, 2022 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Baobab Queens ya Dodoma na kufunga bao lake la kwanza mchezo ukimalizika kwa sare ya 1-1.

Akafunga tena kwenye mchezo wa pili wa kirafiki dhidi ya Ceassia Queens ya Iringa Oktoba 14, 2022 dakika ya 50 kwenye ushindi wa mabao 2-0, kisha akang’ara tena Oktoba 22 akifunga bao la ushindi dhidi ya Yanga Princess mchezo maalum wa tamasha la wanawake Simba Queens ikishinda 2-0.

Ndani ya miezi mitano akiwa Simba Queens, Jentrix amecheza mechi 12 za Ligi Kuu sawa na dakika 1,080 na kufunga mabao 13 likiwamo moja la penalti.

MABAO MANNE

Jentrix ni mchezaji pekee hadi sasa kwenye Ligi hiyo ambayo iko raundi ya 14 ambaye amefunga mabao manne katika mchezo mmoja.

Alifanya hivyo dhidi ya Alliance Girls kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa Februari Mosi, 2023 wakati Simba Queens ikishinda mabao 4-0 ambapo alifunga dakika ya nane, 25, 43 na 64.

NNE BILA BAO

Alikosa mechi mbili za kwanza za ligi kwa timu yake dhidi ya JKT Queens na The Tigers, lakini baada ya hapo ameanza mechi zote 12 huku mechi nne tu ndizo hakufanikiwa kufunga bao.

Jentrix hakufunga bao katika mechi tatu mfululizo, dhidi ya Yanga Princess ulioisha kwa sare ya 1-1 ikiwa ni mechi yake ya kwanza kwenye ligi, Fountain Gate Princess na Mkwawa Princess kisha akashindwa kufunga mbele ya Ceassia Queens baada ya kufunga mfululizo kwenye mechi tatu.

MECHI NANE

Tangu alipoanza kuifungia bao timu yake kwenye ligi, Jentrix amefunga mfululizo mechi saba akifanya hivyo dhidi ya Amani Queens, Alliance Girls, Baobab Queens, JKT Queens, The Tigers, Yanga Princess, Fountain Gate na Mkwawa huku akiwa hajaifunga timu moja tu ya Ceassia.

YANGA WANAMJUA

Msimu huu, Simba Queens imekutana na Yanga Princess katika mechi tatu, zikiwamo mechi mbili za ligi na moja ya mashindano maalum ya kuadhimisha tamasha la michezo kwa wanawake nchini.

Amecheza michezo yote mitatu na kufunga katika miwili akiifunga Yanga Princess mabao mawili likiwamo la ushindi lililowapa ubingwa kwenye mchezo wa tamasha.

Aliifunga Yanga Princess Oktoba 22, 2022 mchezo wa kusaka bingwa wa tamasha la wanawake katika Uwanja wa Mkapa, dakika ya 88 na kuipa Simba Queens kombe hilo. Akaifunga kwenye ligi katika mchezo wa raundi ya pili iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, Machi 22, 2023 mnamo dakika ya 30 ukiisha kwa sare ya 1-1.

OPPAH, CYNTHIA WAMLAINISHIA

Jentrix ni kinara wa mabao ligi hiyo akiwa na 13 katika michezo 12 aliyocheza za ligi hiyo ambapo Simba Queens imefunga mabao 40 katika mechi 13. Wanaomfuatia ni Cynthia Musungu (Fountain Gate Princess), Donisia Minja (JKT Princess) na Oppah Clement (Simba Queens) wenye mabao tisa.

Wengine kwenye mbio hizo ni Winfrida Charles wa Alliance Girls aliyefunga mabao nane, Asha Djafari wa Simba Queens, Jamila Rajabu (Boabab) na Stumai Abdallah (JKT Queens) wenye mabao sita.

Hata hivyo, njia ni nyeupe kwa kinara huyo wa mabao kutwaa kiatu cha dhahabu mwishoni mwa msimu baada ya washindani wake wa karibu kwenye mbio hizo, Oppah na Cynthia kutimkia barani Ulaya.

Wachezaji hao waliondoka baada ya mzunguko wa kwanza SWPL kukamilika (raundi tisa) ambapo Oppah amesajiliwa na Beskitas ya Uturuki huku Cynthia akienda zake Kryvbas ya Ligi Kuu nchini Ukraine.

DAKIKA ZAKE

Tangu kutua bongo Septemba, 2022, Jentrix ameichezea Simba Queens michezo 15 akifunga mabao 16, ambapo 13 ni ya Ligi Kuu na matatu ni ya kirafiki huku akionekana kuwa hatari zaidi kuanzia dakika ya 50 hadi 90.

Katika hayo, mabao nane ameyafunga kipindi cha pili dakika za 50, 53, 60, 64, 70 na 88 huku sita akiyapachika katika kipindi cha kwanza mnamo dakika ya 5, 8, 11, 25, 30 na 43.

HISTORIA, MAFANIKIO

Mkali huyo wa mabao alizaliwa November 27, 2001 huko Kakamega, Kenya ambapo aliichezea Vihiga Queens na kuisaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Kenya misimu mitatu mfululizo mwak 2017, 2018 na 2019.

Januari, 2022 alijiunga na klabu ya Fatih Karagumruk SK ya Uturuki na kuisaidia kumaliza nafasi ya pili katika ligi nchini humo akifunga mabao 19 katika msimu wa 2021-2022.

Mafanikio mengine ni kubeba ubingwa wa Cecafa mwaka 2019 akiwa na timu ya taifa ya Kenya na kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo huku akiisaidia Vihiga Queens kuwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ukanda wa Cecafa mwaka 2021 na kukata tiketi ya kushiriki michuano hiyo barani Afrika.

Akizungumzia kiwango chake kwenye kufumania nyavu, Jentrix anasema; "Hii inachochewa na wachezaji wenzangu ambao tumejuana kwa haraka na kila mtu, mnapoelewana inakuwa rahisi kucheza nao, kwahiyo tangu nimekuja napata sapoti ya kila mtu lakini pia inaletwa na bidii ninayoiweka kuhakikisha kila ninapopata nafasi nafunga,"

"Nilikuja Tanzania kucheza Champions League lakini sikupata nafasi, nikasema nisubiri ligi huko ndiko nitakapooneka na nili-promise nitakuwa top striker, Ligi ni ngumu ina ushindani kila timu inahitaji ubingwa nawaambia mashabiki waendelee kuwa pamoja nasi katika michezo iliyobaki tunaamini tutafanya makubwa zaidi."

Chanzo: Mwanaspoti