Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Saleh Ally 'Jembe' amesema kuwa vilabu vya Tanzania havina uwezo wa kumlipa mchezaji mshahara wa Tsh milioni 40 kwa mwezi.
Jembe amesema hayo kufuatia vuguvugu la Klabu ya Yanga na mchambuliaji wao raia wa Congo DR, Fiston Mayele ambaye inaelezwa kuwa ameomba kulipwa mshahara wa tsh milioni 40 ili aendelee kusalia klabuni hapo msimu ujao.
"Sio Simba wala Yanga, hakuna timu hapa nchini yenye uwezo wa kumlipa mchezaji mshahara wa dola 17,000 (zaidi ya Tsh milioni 40) kwa mwezi. Hii wanalipwa makocha, tena makocha wachache sana labda wa Timu ya Taifa ila kwa mchezaji sio rahisi.
"Mimi naamini kwa Simba na Yanga kulipa kiasi hicho ni ngumu lakini kwa Wydad, Al Ahly, Zamalek au Pyramids wanaweza kumnunua mchezaji hata dola milioni 1 ambapo kwa Tanzania unasajili nusu ya kikosi chako.
"Nadhani Mayele angewapunguzia bei yanga ili afanye nao kazi vizuri ili msimu ujao hata akiondoka kwenda kutafuta pesa nje sio mbaya," amesema Saleh Jembe.