Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jay Jay Okocha anogesha mjadala ishu ya uraia pacha

Okocha (18).jpeg Jay Jay Okocha anogesha mjadala ishu ya uraia pacha

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Nyota wa zamani wa Nigeria, Jay Jay Okocha ametoa ushauri kwa Tanzania kuhakikisha inakuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa katika ligi kubwa na zenye ushindani Ulaya ili timu za taifa zifanye vizuri.

Okocha ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho suala la uraia pacha limeanza kuliliwa na wadau wengi wa mpira wa miguu likionekana kama chachu ya Timu za Taifa za Tanzania kufanya vizuri kimataifa.

Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa mashindano ya dunia ya soka kwa klabu za veterani ambayo kwa mara ya kwanza yatafanyika Kigali, Rwanda, Septemba mwakani, Okocha alisema mwamko wa soka Tanzania unapaswa kwenda sambamba na uwepo wa idadi kubwa ya wanasoka wanaocheza nje hasa katika ligi kubwa.

Kwa mujibu wa Okocha, wachezaji wa Kiafrika wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi na kulifanya soka la bara hili kupigia hatua kwa kuhamishia ubora na ushindani wanaopata huko hadi katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) na Kombe la Dunia.

“Tanzania ina vipaji vingi vya soka. Kuunganisha vipaji hivi na kupandisha timu ya taifa kwenda ngazi za juu tunahitaji kuona wachezaji wengi wa Tanzania wanashindana katika ligi kubwa za Ulaya.

“Uwezo wa kushindana, uzoefu wa kimataifa na mazingira ya ushindani ya ligi za Ulaya vinaweza kuendeleza ujuzi wao wa mpira wa miguu,” alisema Okocha.

Okocha alisema  historia inaonyesha mataifa mengi ya Afrika ambayo wachezaji wake wanacheza katika ligi za Ulaya, yamekuwa yakipata mafanikio makubwa pindi kunapokuwa na mashindano ya kimataifa.

“Kwa wachezaji wengi kuwa kwenye ushindani katika ligi kubwa Ulaya, kikosi cha Tanzania kitanufaika kwa kuongezeka ushindani, ngazi ya juu ya uelewa wa mbinu na uzoefu wa kimataifa wa staili tofauti za uchezaji,” alisema Okocha.

Tanzania ina wachezaji watatu tu wanaocheza ligi zenye ushindani Ulaya ambao ni nahodha Mbwana Samatta anayeitumikia PAOK ya Ugiriki, Novatus Miroshi anayechezea Shakhtar Donetsk ya Ukraine na Kelvin John aliyepo Genk ya Ubelgiji.

Uchache wa wachezaji wa Kitanzania wanaocheza ligi za ushindani Ulaya umechangia kushawishi wadau wengi wa soka kuomba kuruhusiwa kwa uraia pacha ili kuvutia baadhi ya wachezaji wenye asili ya Tanzania waliopo katika nchi mbalimbali Ulaya ili waweze kuichezea Taifa Stars.

Kilio hicho cha wadau kilipelekea wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutoa agizo kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Katiba na Sheria na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukutana pamoja ili kuangalia namna ya kutengeneza mazingira rahisi kwa Taifa Stars kuvutia wachezaji wenye asili ya Tanzania kuichezea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live