Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jamus, JKU zaongezwa Mapinduzi Cup

JKU ZNZ Jamus, JKU zaongezwa Mapinduzi Cup

Mon, 25 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu za Jamus kutoka Sudan Kusini na vinara wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), JKU zimeongezwa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 itakayoanza rasmi Alhamisi kuchukua nafasi za Bandari FC ya Kenya na URA zilizojitoa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukosa vibali vya kuja nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024, Mbarouk Othman amesema mapema leo mjini Unguja kuwa, Bandari iliyokuwa Kundi C na ilipangwa kukata utepe wa michuano hiyo Desemba 29 kwa kuvaana na Vital'O ya Burundi, huku URA yenyewe ingefungua michuano Desemba 28 dhidi ya watetezi Mlandege ya Zanzibar nafasi zao zinazibwa na timu hizo mbili mpya ili michuano iendelee kama kawaida.

Kutokana na mabadiliko hayo, idadi ya timu zinabaki kuwa 12, lakini maeneo yanayotoka yatatofautiana na awali ambapo ilikuwa imelenga timu nne za kigeni, nne za Tanzania Bara na nne za visiwani Zanzibar, ila kwa sasa itakuwa ni timu nne za Bara, tatu za kutoka nje ya nchi na tano za Zanzibar.

Timu za kigeni ni Vital'O ya Burundi, APR ya Rwanda na Jamus ya Sudan Kusini, huku za Bara zikibaki zile zile za Simba, Yanga, Azam FC na Singida Fountain Gate wakati za visiwani Zanzibar ni JKU, KZV na watetezi Mlandege za kutokea Unguja wakati za visiwani Pemba ni Chipukizi na Jamhuri.

Huu ni msimu wa 18 wa michuano hiyo tangu ilipoasisiwa kwa msimu wa sasa mwaka 2007, huku Azam ikiwa ndio timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi ikibeba mara tano, ikifuatiwa na Simba yenye mataji manne na kuwa kinara wa kucheza fainali nyingi hadi sasa zikiwa ni nane, ikifuatiwa na Azam FC na Mtibwa Sugar zilizocheza mara sita kila mojas.

Michuano hiyo inayoenda sambamba na Miaka 60 ya maadhimisho ya Mapinduzi Zanzibar  yaliyofanyika Januari 12, 1964 ambapo kama kawaida fainali za msimu huu zitafanyika Januari 13.

Msimu uliopita Mlandege ilibeba taji hilo kwa kuifunga Singida kwa mabao 2-1 timu hiyo wakati huo ikiwa chini ya Kocha Abdallah Mohammed 'Baresi' aliyepo Mashujaa FC kwa sasa inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live