Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jamie Carragher, Gary Neville watofautiana EPL

Carragher X Neville Jamie Carragher, Gary Neville watofautiana EPL

Wed, 21 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Magwiji, Jamie Carragher na Gary Neville wamefichua utabiri wao wa Ligi Kuu England itakavyokuwa msimu huu huku wakipishana kwenye baadhi ya mambo kibao juu ya machaguo yao.

Wawili hao waliokuwa mahasimu wakubwa enzi zao walipokuwa wakicheza, mmoja akiwa Liverpool na mwingine Manchester United, waliweka bayana utabiri wao wa msimu huu wa Ligi Kuu England, kipindi kinachorushwa na Sky Sports cha Monday Night Football.

Wametofuatiana kwenye mambo mengi ikiwamo timu itakayochukua ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu wa 2024-25.

Carragher anaamini Manchester City itanyakua taji la tano mfululizo la ligi hiyo, lakini Neville anaamini Arsenal itaipiku timu hiyo ya Pep Guardiola na kulipeleka taji hilo huko Emirates.

Beki huyo wa zamani wa Man United, Neville aliambia Sky Sports: "Wanazidi kuwa wazuri, wanazidi kukaribia kwenye ubora unaopaswa, sifahamu itakuwaje, lakini naona kabisa watafanya. Naona kuna namna watafanya. Inaweza isiwe uhakika wa asilimia 100 kutokana na vile Pep Guardiola amekuwa akifanya mambo yake, anashinda kila wakati. Lakini, naamini Arsenal wanakaribia kwenye anga hizo na wamekuwa wakidumu kwenye kiwango bora kabisa cha soka lao kwa miaka sasa."

Vigogo hao walipishana pia kwenye utabiri wao wa timu gani itakuwamo kwenye Top Four ya msimu huu. Carragher amejichagua Arsenal, Liverpool na Tottenham zitaungana na mabingwa Man City kwenye Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu.

Lakini, Neville kwa upande wake ameziingiza Man United na Chelsea zitaungana na Arsenal na Man City katika idadi ya timu nne za juu ambazo zitanyakua tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.

Hapo ndipo gwiji wa Liverpool, Carragher alipoanza kuhoji nguvu ya Neville kuiondoa miamba hiyo ya Anfield inayonolewa na Arne Slot kwenye orodha ya timu zitakazomaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi.

Neville alisema: "Kama ukitazama wachezaji wa safu ya kiungo ya Manchester United, kisha ukaangalia viwango vya makocha, hupati majibu ya haraka Erik ten Hag na Arne Slot watakavyoenda kuchuana.

"Sidhani Liverpool ya viungo Endo, Szoboszlai na MacAllister wamefanya kitu kikubwa sana na Slot atapata huduma bora kutoka kwa wakali hao kuliko kipindi alichokuwa Jurgen Klopp. Swali langu ni kama kiungo hiyo itaweza kupambana kwa msimu wote. Nasubiri wanithibitishie.

"Nadhani Manchester United imeongeza viungo zaidi. Nadhani ina machaguo mengi na imekuwa na wachezaji wazuri eneo hilo.

"Kobbie Mainoo, ameingia kwenye eneo hilo, atacheza sambamba na Casemiro, Fernandes na yupo pia Mason Mount na Scott McTominay."

Neville aliongeza: "Kwa mtazamo wangu kuondoka kwa Klopp kutaacha madhara makubwa pia."

Nje ya Top Four, Carragher amezitaja Man United na Aston Villa zitamaliza kwenye nafasi ya tano na sita, wakati Neville kwa upande wake amezitaja Liverpool na Tottenham kwenye nafasi hizo zinazotoa tiketi ya kucheza michuano ya Europa League.

Carragher ameitaja West Ham United kwenye vita hiyo ya kufukuzia tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya, wakati Neville chaguo lake ni Newcastle. Wawili hao wamekubaliana kwenye ishu ya mfungaji bora, ambapo wote wamemchagua straika Erling Haaland wa Man City.

Wawili hao walikubaliana pia kwenye timu mbili kati ya tatu zitakazoshuka daraja, ambazo ni Southampton na Leicester City.

Neville anaamini timu zote tatu zilizopanda daraja msimu huu ndizo zitakazoshuka, wakati Carragher anaamini Ipswich Town itapona na badala yake Nottingham Forest ndiyo itakayoshuka daraja.

Carragher anaamini fowadi mpya wa Chelsea, Pedro Neto utakuwa usajili bora zaidi msimu hu, wakati Neville anaamini staa mpya wa Spurs, Dominic Solanke utakuwa usajili wenye mchango mkubwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Neville anaamini beki wa Arsenal, Jurrien Timber ndiye mchezaji wa kumtazama zaidi msimu huu, wakati Carragher shilingi yake yeye kwenye la mchezaji atakayevutia kumtazama ipo kwa staa mpya wa Brighton, Yankuba Minteh kutoka Gambia.

Mwisho kabisa, Carraghe amemchagua kocha mkuu wa Liverpool, Slot kuwa ndiye wa kumtazama zaidi msimu huu, wakati Neville amewataka Enzo Maresca wa Chelsea na Erik ten Hag wa Man United, kuwa ndio makocha wa kuwatazama zaidi msimu huu wa 2024-25.

Chanzo: Mwanaspoti