Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jahazi la Ruvu lazidi kuzama

Ruvu Shooting Majanga Tena Jahazi la Ruvu lazidi kuzama

Mon, 25 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Majanga yamezidi kuiandama Ruvu Shooting, baada ya jahazi la timu hiyo kuzama tena juzi licha ya kuwa nyumbani mjini Iringa kwa kufungwa mabao 2-1 na Stand United na kuweka mguu mmoja wa kushuka daraja kutoka Ligi ya Championship kwenda First League kwa msimu ujao.

Ruvu iliyoshuka kutoka Ligi Kuu Bara msimu uliopita, inaendelea kuburuza mikia kwa kusaliwa na pointi 11 baada ya mechi 26, ikibakiwa na michezo minne ambayo hata kama itashinda zote itaifanya ifikishe pointi 23 ambazo hazitoi timu hiyo katika msala wa kushuka.

Kanuni za ligi inasema, timu zinazoshika nafasi mbili za mwisho hushuka daraja moja kwa moja na zile zinazoshika nafasi ya 13 na 14 zinacheza play-off ya kusaka nafasi ya kuvaana na timu zitakazoshika nafasi ya tatu na nne zitakazochujana katika First League.

Hesabu zilivyo, Ruvu katika mechi nne za mwisho za kushuka daraja iwe ni moja kwa moja au kupitia play-off inaihusu, licha ya juzi kucheza soka tamu na kutangulia kupata bao mapema dakika ya tisa la Faraj Kayanda ambalo hata hivyo halikuisaidia kuepuka kipigo mbele ya Chama la Wana.

Stand United iliyowahi kutamba Ligi Kuu kama ilivyokuwa kwa Ruvu, ilichomoa bao hilo dakika ya 40 kupitia kwa Charles Warsha aliyefunga kwa kichwa katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Samora kabla ya Pascal Peter kutumia bao la ushindi dakika nne kabla ya filimbi ya mwisho.

Mfungaji huyo alikwamisha mpira huo pia kwa kichwa akimalizia friikiki na kuwahi mpia kabla ya kuokolewa na mabeki wa Ruvu waliojisahau.

Ushindi huo umeifanya Stand kufikisha pointi 30 na kupanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya 10 ikiendelea kupambana kuepuka janga la kushuka daraja.

Katika mechi nyingine iliyopigwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea, TMA ya Arusha ilipata ushindi muhimu mbele ya wenyeji FGA Talents wa bao 1-0 na kuchupa hadi safasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 51.

Bao pekee lililowazamisha wenyeji lilitumbukizwa wavuni dakika ya 28 na kipa wa FGA Talents, Mussa Webilo aliyejifunga katika harakati za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na mshambuliaji wa TMA naye kuusukumia wavuni kwa miguu.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo miwili na maafande wa Transit Camp iliyotoka kuwanyoa Pan Africans katika mechi iliyopita itavaana na mabingwa wengine wa zamani wa Tanzania, Cosmopolitan, huku Mbeya Kwanza itakuwa na kazi mbele ya Biashara United.

Cosmo ilikuwa timu ya pili nchini kubeba ubingwa wa Bara mwaka 1967 baada ya Simba kubeba mara mbili mfululizo tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965 na kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 30 (kabla ya mechi za jana).

Chanzo: Mwanaspoti