Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKU yawalainishia Waarabu CAF

JKU 2024 JKU yawalainishia Waarabu CAF

Thu, 8 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Yanga ikipata mtelezo kutoka kwa Vital'O ya Burundi iliyoamua mechi za nyumbani ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024-2025 kucheza Dar es Salaam, JKU ya Zanzibar nayo imewalainishia wapinzani wao Waarabu wa Misri, Pyramids.

Ipo hivi. Mabingwa hao wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) na wawakilishi wa visiwa hivyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, imepangwa kucheza raundi ya kwanza dhidi ya Pyramids ya Misri, mchezo wa kwanza ukipangwa kufanyika Agosti 18 mwaka huu kisha marudiano Agosti 23 mwaka huu.

Awali Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitoa orodha ya viwanja vitakavyotumika kwa mashindano ya ngazi ya klabu msimu wa 2024-2025 vilivyokidhi vigezo na kuuondoa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar, lakini baadaye Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) likathibitisha uwanja huo umeruhusiwa kutumika hivyo wawakilishi wao JKU kupitia Ligi ya Mabingwa na Uhamiaji inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika wangeutumia.

Licha ya kuruhusiwa kuutumia uwanja huo, Mwanaspoti limepata taarifa kwamba JKU imepanga mechi zao zote kuchezea ugenini, huko Misri.

Kocha wa JKU, Salum Haji, ameliambia Mwanaspoti kuwa, uamuzi wa klabu hiyo kwenda kucheza mechi zote za CAF nchini Misri kumetokana na udhamini walioupata.

"Ni kweli mechi zetu zote mbili tutachezea Misri baada ya kupata mdhamini ambaye amegharamikia safari nzima ikiwemo kambi ikiwemo kututafutia uwanja wa mazoezi sambamba na kufanya utalii tukiwa huko, lakini pia benchi la ufundi tumepata nafasi ya kwenda kufanya kozi nchi yoyote tutakayochagua. Pia akademi yetu ya JKU ipo katika udhamini huo," amesema Haji maarufu kama Kocha Msomi aliyeongeza;

"Agosti 15 jioni tunatarajia kusafiri kwenda Misri kwa mchezo wa mkondo wa kwanza utakaochezwa Agosti 18, sisi tutakuwa wenyeji, kisha ile ya pili wenyeji ni Pyramids itachezwa Agosti 23. Mechi zote hizo zitachezwa usiku."

Kwa upande wa Uhamiaji, Ofisa Habari wa timu hiyo, Mwinyi Hamadi, amesema hadi sasa wao mechi yao ya nyumbani itachezwa Uwanja wa New Amaan Complex, lakini kunaweza kutokea mabadiliko kutokana na uwepo wa mazungumzo ya kwenda kuchezea Libya mechi zote mbili.

"Maandalizi yetu yanakwenda vizuri kuelekea mchezo wetu wa CAF dhidi ya Al Ahli Tripoli, uwepo wa taarifa za kwenda Libya kucheza mechi zote mbili zipo lakini bado hatujafikia makubaliano mpaka sasa, kama kutakuwa na lolote tutakaloamua tutatoa taarifa rasmi mapema kabla ya kufika siku ya mchezo," amesema.

Kwa mujibu wa ratiba ya CAF, mshindi wa mchezo kati ya JKU dhidi ya Pyramids, atacheza raundi ya pili dhidi ya mshindi kati ya Azam dhidi ya APR kusaka hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mshindi baina ya Uhamiaji na Al Ahli Tripoli atacheza raundi ya pili dhidi ya Simba kuwania makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti