Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKU ni mwendo wa uji wa mtama, tende

Kocha JKU Afunguka Ishu Ya Feisal Salum JKU ni mwendo wa uji wa mtama, tende

Fri, 13 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati timu nyingi za Bara zikitumia saa moja kufanya mazoezi kujiandaa na mashindano yoyote, Zanzibar hasa kwa timu za jeshi ni tofauti wao ni masaa mawili na nusu.

Iko hivi; kikosi cha JKU ambacho amekuwa akifanya mazoezi staa wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kilicho chini ya kocha Khamis Rashid kinafanya mazoezi masaa mawili hadi matatu.

Mwanaspoti lilishuhudia wanajeshi hao wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa JKU Saaten juzi walianza saa 2:15 kutokana na hali ya hewa kawaida huwa wanaanza saa 12:00.

Kikosi hicho kilichosheheni wazawa kilianza mazoezi mepesi ya kupasha misuli kwa kukimbia taratibu kwa nusu saa na baadaye kucheza mpira wa kupasiana pasi fupifupi wakimweka mtu kati walitumia nusu saa jumla saa moja.

Baada ya hapo kocha aligawa timu mbili na kuruhusu mpira kuchezwa nusu uwanja ambapo walicheza saa moja huku timu zote mbili zikionekana kutumia nguvu kuhakikisha zinafika eneo la wapinzani.

UJI WA MTAMA, MAANDALIZI

Wakati timu za Bara zikionekana kutumia ndizi mbivu baada ya kutumia nguvu nyingi kucheza, Zanzibar ni tofauti wao ni mwendo wa uji wa mtama.

Mastaa hao baada ya mazoezi makali na ya muda mrefu walionekana kutoka uwanjani na kukaa pembezoni mwa uwanja wakiwa na bakuri kubwa mkononi na maandazi.

Mwanaspoti lilifanya juhudi ya kuongea na kocha ili kufahamu kwanini uji na sio ndizi alisema wao wanakunywa uji wa mtama ambao umekuwa ukirudisha nguvu haraka zaidi. “Huu uji ni mzuri sana kwa wachezaji baada ya mazoezi unaongeza nguvu kwasababu una sukari, pia tuna utaratibu wa kula tende leo hazipo lakini mara nyingi ni uji na tende."

SABABU ZA MAZOEZI SAA MBILI

“Wachezaji wetu hawakai kambini, wakitoka hapa wanarudi majumbani kwao hiyo tunaamua kutumia muda mrefu ili kuwachosha wakitoka hapa wanarudi kulala wanakuwa hawana hamu ya kufanya kitu kingine chochote,” alisema na kuongeza;

“Pia inafuatana na program, makocha tupo tofauti lakini kozi tunazosoma mazoezi ni saa mbili japo kila kocha ana aina yake ya ufundishaji kulingana na kile anachokizingatia zaidi.”

Anasema pia Bara wanafanya muda mchache kwa sababu wanakuwa na program mbili wanaweza kufanya asubuhi na jioni lakini wao ni asubuhi tu.

AMTAJA FEI TOTO

Wakati huohuo Mwanaspoti lilitaka kufahamu kwanini Fei Toto hajaonekana kwenye mazoezi hayo wakati amekuwa akifanya nao pamoja, alisema sio mchezaji wao hawana sababu ya kumchunga kuhakikisha anaonekana mazoezini lakini juzi (Jumanne) alifanya nao mazoezi na kuwaambia hatakuwa nao pamoja juzi kwa sababu anataka kwenda kufanya mazoezi ya mchangani.

“Fei Toto huwa hatumlazimishi kuja hapa anakuja yeye mwenyewe kwa sababu ni timu aliyotoka na amekuwa akifanya mazoezi nasi anapojisikia kwa sababu siyo mchezaji wetu hatuwezi kulazimisha aje hapa,” alisema na kuongeza;

“Uwepo wake unaongeza kitu kwenye mazoezi yetu kwa sababu ni mchezaji mzuri na mzoefu mastaa wetu wamekuwa wakijifunza kitu kutoka kwakwe.”

MNIGERIA AIBUKA MAZOEZINI

Baada ya kushindwa kuonyesha kiwango kizuri Coastal Union alikoenda kwa ajili ya kufanya majaribio beki wa kati kutoka Nigeria Emmanuel Vicent alionekana kwenye mazoezi ya JKU juzi.

Staa huyo ambaye alitengewa mazoezi yake binafsi alionekana kufanya mazoezi mepesi na kukimbia kwa muda aliliambia gazeti hili kuwa ametoka timu ya Reven FC.

“Nipo hapa kwa ajili ya kuichezea timu hii, Nigeria nimetokea Reven FC naamini nitapata nafasi nzuri ya kucheza na kuonyesha uwezo nilionao,” alizungumza hayo machache na kuendelea na utaratibu wa kunywa uji.

Chanzo: Mwanaspoti