Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKU inautaka ubingwa, yampiga mtu wiki ZPL

JKU Bao 7 JKU inautaka ubingwa, yampiga mtu wiki ZPL

Sat, 18 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Saa 24 tu, tangu maafande wa KVZ walipoifumua Maendeleo 7-3 katika mechi ya Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), vinara wa ligi hiyo, JKU imejibu mpigo jana jioni Ijumaa kwa kuinyoosha Jamhuri ya Pemba kwa mabao 7-0 ikionyesha kiu ya kubeba ubingwa kwa msimu huu.

JKU ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Amaan Kwa Wazee, mjini Unguja na kuzidi kujiweka pazuri katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo unaoshikiliwa kwa misimu mitatu mfululizo kwa sasa na Mabaharia wa KMKM, kwani imefikisha pointi 53 kupitia mechi 24.

Pointi ilizofikisha JKU inayoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa muda mrefu tangu duru la kwanza, imeifanya iziache KVZ na Zimamoto kwa tofauti ya alama sita, kwani timu hiyo zilizopo ndani ya Tatu Bora sasa zenyewe zina 47 kila moja, japo Zimamoto imecheza michezo 23.

Kipigo hicho kwa Jamhuri, kimezidi kuiweka pabaya katika janga la kushuka daraja, kwani imeganda nafasi ya 15, ikiwa na pointi 18, tatu zaidi na ilizonazo Maendeleo inayoburuza mkia kwa sasa.

Katika mchezo huo, Mudrik Miraji Mawia alikuwa mchezaji wa nne kwa msimu huu kufunga hat trick baada ya kutupia kambani mabao matatu akifuata nyayo za Ibrahim Hamad 'Hilika' wa Zimamoto, Ibrahim Is-haka wa KMKM na Suleiman Mwalim Abdalla wa KVZ ambaye jana Alhamisi alifunga mabao manne na kuweka rekodi ya kuwa nyota pekee aliyefunga idadi hiyo katika mechi moja.

Mawia alianza kutupia kwa kuifungia JKU bao la kwanza dakika ya 19 kabla ya Saleh Masoud Abdulla kuongeza mengine mawili dakika ya 22 na 27, kisha Mawia kufunga tena bao la nne la timu hiyo katika mchezo huo na la pili kwake dakika ya 37.

Mabao hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko, licha ya wachezaji wa Jamhuri kucharuka na kusaka angalau bao la kufutia machozi bila mafanikio kutokana na ngome ya JKU kuwa imara.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kuingia uwanjani kwa kasi na kutengeneza mashambulizi makali, lakini ni wenyeji JKU walionufaika kwa kuongeza mabao mengine matatu yaliwekewa kimiani na Mudrik Abdi Shehe aliyefunga mawili dakika ya 49 na 79, kabla ya Mawia kupigilia msumari wa mwisho dakika ya 84 na kukamilisha hat trick yake katika pambano hilo.

Mabao hayo matatu yamemfanya nyota huyo afikishe manne, huku Mudrik Abdi Shehe akifikisha saba, ilihali Saleh Masoud Abdulla akifikisha sita hadi sasa katika ligi hiyo iliyosaliwa na mechi za raundi sita kabla ya kufikia tamati Juni 17 mwaka huu.

Katika pambano jingine lililopigwa pia jioni ya leo kwenye Uwanja wa Mao A, Mafunzo iliwatambia maafande wenzao wa Uhamiaji kwa kuwafunga bao 1-0, lililowekwa kimiani na Matheo Andrea dakika ya kwanza ya mchezo huo uliokuwa mkali.

Ushindi huo umeifanya Mafunzo kuchupa kwa nafasi mbili katika msimamo wa ligi hiyo, ikitoka ya saba hadi ya tano kwa kufikisha pointi 37 zilizotokana na michezo 24, huku Uhamiaji ikibaki nafasi ya nane ikiwa na pointi 29 kwa idadi ya mechi 23 ilizocheza hadi sasa.

Bao hilo pekee na la mapema kwa Matheo ni la nne kwa mchezaji huyo katika ligi hiyo kwa msimu huu hadi sasa.

Chanzo: Mwanaspoti