Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKT sasa yahamia Azam Complex

Azam Complex Rev JKT sasa yahamia Azam Complex

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kitendo cha JKT Tanzania kuuchagua Uwanja wa Azam Complex uliopo Dar es Salaam kwa michezo yote ya nyumbani msimu huu baada ya ule wa Kambarage, Shinyanga kuzuiwa kwa kukosa vigezo, kumeifanya klabu ya Azam kuendelea kuvuna maokoto kupitia huo uliopo Chamazi.

Mwenyekiti wa JKT Tanzania, Godwin Ekingo aliliambia Mwanaspoti, wamepokea barua kutoka Bodi ya Ligi (TPLB) ya kufungiwa kwa Uwanja wa Kambarage waliokuwa wakiutumia kwa mechi za awali za msimu huu na sasa wameamua kuuchagua Azam Complex kwa mechi zilizosalia wakiwa nyumbani.

“Tumechagua Azam Complex katika michezo ya nyumbani hadi pale tutakapotoa taarifa nyingine hivyo tunawaomba tu mashabiki zetu waendelee kutusapoti kama mwanzo japo tunatambua kitendo cha kuhama tena kimewaumia kwa kiasi kikubwa,” alisema Ekingo.

JKT inakuwa timu ya pili mbali na Azam FC kuutumia uwanja huo katika michezo ya nyumbani msimu huu baada ya Yanga, inayoutumia huku mchezo wa kwanza kwa timu hiyo ya mafande utakuwa ni dhidi ya Tabora United utakaopigwa Oktoba 25, saa 10:00 jioni.

Kitendo cha JKT kuutumia uwanja huo, inaifanya Azam ijihakikishie kuingiza Sh5.9 milioni kama gharama za kuchezea kwa timu za Tanzania, huku zile za nje ya nchi zikitozwa Sh11.7 milioni na hii iwe kwa mechi za mchana au usiku.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live