Kikosi cha JKT Tanzania leo kinatarajia kuanza safari kuelekea mkoani Morogoro katika mchezo wao dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa Februari 25 katika Uwanja wa CCM Gairo.
Ikumbuke kuwa JKT ni vinara wa ligi ya Championship wakiongoza kwa alama 46, huku Fountain Gate ikiwa nafasi ya 5 na alama 32 .
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu wa JKT Tanzania, Kapteni Speratus Lubinga alisema kuwa jumla ya wachezaji 28 na viongozi 9 watakuwa katika msafara huo.
"Tunatambua vyema ubora wa Fountain Gate lakini ninaimani na kikosi chetu kinaenda kupambana na kuondoka na alama tatu kwa kufuata maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa ambaye alitaka kuona kikosi kinarejea ligi kuu msimu ujao, sina shaka na wachezaji wangu kwani wanajituma kuhakikisha inarudi ligi kuu," alisema
Alifafanua kuwa viongozi pamoja na benchi la ufundi wamejipanga kuhakikisha wanafanya vyema kwa kufuata maagizo ya Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkuu wa utawala Brigedia Hassan Mabena, pamoja na Mlezi wa timu Luteni Kanali Godfrey Mvula kuhakikisha kikosi kinashiriki ligi kuu msimu ujao.
"Kikosi changu kimejipanga vyema kuhakikisha tunavuna alama 3 ugenini na baadaye kinaendelea na mchezo mwingine wa Michuano ya FA utakaochezwa Uwanja wa Liti mkoani Singida sina shaka na kikosi changu ambacho kipo chini ya kocha Malale Hamsini kwa sasa kila mchezo ni fainali na wachezaji wanapambana kuhakikisha wanapata ushindi michezo iliyobaki," alisema
Alisema kikosi kipo tayari na hakuna majeruhi na wapo imara kupambana michezo ya ligi na FA dhidi ya Singida Big Stars utakaochezwa Machi 4 mwaka huu.