Timu ya maafande ya JKT Tanzania huenda ikajiweka mtegoni katika Ligi Kuu Bara kutokana na kujiandaa kuwakosa wachezaji zaidi ya tisa wa kikosi cha kwanza akiwemo Shiza Kichuya kwa muda wa miezi mitatu kutokana na nyota hao kuwa kwenye hatua za mwisho za kwenda kuanza mafunzo ya kijeshi.
Kocha wa JKT TZ, Malale Hamsini amethibitisha hilo huku akiwekas bayana mpango maalum uliosukwa na benchi la ufundi la timu hiyo ili kuwasaidia kufanya vizurio kwenye mechi zilizopo mbele yao bila ya kuwa na nyota hao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Malale alisema; "Ni kweli wachezaji hao wanaenda kwenye kozi, ni kitu ambacho tulikuwa tunakitarajia, hivyo wengine ambao tutaendelea nao kikosini, hivyo sidhani kama hili linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mipango yetu. JKT tuna wachezaji wengi na wapo tayari kutumika, tutatoa nafasi na naamini kwamba watakuwa msaada kwenye timu kwa kipindi chote ambacho tutawakosa wenzetu."
Katika mchezo wa ligi ambao JKT Tanzania ilipoteza dhidi ya Simba kwa bao 1-0 walilofungwa na Clatous Chama, wachezaji sita wa kikosi cha kwanza walikuwa na upara kichwani tayari kwa ajili ya kwenda kwenye mafunzo hayo huku watatu wakiwa sehemu ya wachezaji wa akiba na wengine wakiwa jukwaani.
Mbali na Kichuya baadhi ya wachezaji wengine ambao watakosekana kwa miezi hiyo mabeki ni; Martin Kiggi, David Brayson, Wema Sadock, kiungo ni Hassan Nassoro, Maka Edward huku kwa washambuliaji akiwemo Sixtus Sabilo.
Katika zoezi ya unyoaji nywele kwa wachezaji hao inaelezwa Kichuya alikuwa kivutio kwani vinyozi walikuwa wakimgombania, akiongelea nafasi hiyo, Kichuya alisema; "Ni kweli tunaenda kozi lakini naamini kuwa wenzetu wataendelea kuipambania timu wakati ambao tutakuwa huko tukiendelea na mafunzo."
Ndani ya miezi mitatu ijayo ukiondoa mchezo wa jana, Jumapili ambao walicheza dhidi ya Namungo, JKT Tanzania itakuwa na kibarua cha kusaka matokeo dhidi ya Yanga, KMC, Kagera Sugar, Mashujaa, Tanzania Prisons, Tabora United, Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar.