Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKT Tanzania haoo Ligi Kuu Bara

JKT Tanzania Wachezaji wa Kikosi cha JKT Tanzania

Fri, 7 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabosi wa timu ya JKT Tanzania wana uhakika chama lao linarudi Ligi Kuu Bara kutokana na kuhitaji pointi nne zitakazowahakikisha kupanda daraja na fasta wameanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi hiyo ukiwa umeshapokea ripoti ya benchi la ufundi kusuka kikosi hicho kwa msimu ujao.

Maafande hao ndio vinara wa Ligi ya Championship wakiwa na pointi 59 na sasa wanahitaji nne katika mechi nne walizosaliwa nazo ili wafikishe 63 ambazo kiuhalisia zitawafanya kupanda daraja.

Timu hiyo itaanza kampeni ya kusaka pointi hizo nne kuanzia Aprili 15 itakuwa ugenini kukipiga dhidi ya African Sports na kama itashinda itakuwa imeweka mguu mmoja ligi kuu ikisaka alama moja tu ili kupanda daraja.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Godwine Ekingo alisema hadi sasa wanaona njia nyeupe ya kurejea wanapopataka, akibainisha tayari kocha mkuu, Malale Hamsini ameanza kupendekeza maeneo ya kuboresha kwa ajili ya ligi kuu msimu ujao.

Alisema kuhusu benchi la ufundi, wamemuachia kocha huyo kuamua wapi paboreshwe na kwamba uongozi upo tayari kwa mabadiliko kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri.

“Mabadiliko kikosini hayo ni lazima japokuwa bado ni mapema kusema nani anatoka au kuingia, kwa sasa tunafikiria mchezo ujao ili kujua hatma yetu na malengo ni kushinda ili kufikia ndoto,” alisema Ekingo.

Kuhusu mafanikio, kigogo huyo alifafanua kuwa kilichowapa matokeo mazuri ni hamasa waliyoitengeneza kikosini kwani kila mchezo kulikuwa na motisha yake na kwamba bado ni endelevu.

Aliongeza kuwa iwapo watafanikiwa kupandia mkoani Tanga, sherehe lazima zifanyikie nyumbani jijini Dar es Salaam na kwamba suti na zawadi kwa timu zimeanza kuandaliwa.

“Hatuwezi kufanyia pati ugenini, lazima tuje nyumbani, hizo suti na zawadi ni kama kawaida lazima viwepo katika kutambua mchango wa wachezaji na benchi la ufundi,” alisema kiongozi huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live