Uongozi wa JKT Tanzania umesema kuwa timu hiyo itaendelea kuwa chini ya Kocha Malale Hamsini itakaposhiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao kutokana na kukoshwa na kazi nzuri aliyoifanya kuipandisha daraja baada ya kusota kwa misimu miwili katika Ligi ya Championship.
Mwenyekiti wa JKT Tanzania, Godwin Ekingo amesema kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kocha mkuu wa kikosi hicho, Malale Hamsini uongozi umeamua kuendelea naye hadi msimu ujao.
“Malale ni mmoja wa makocha wenye uwezo mkubwa hapa nchini na hakuna sababu ya kuachana naye baada ya kumalizika kwa Ligi ya Championship kama ambavyo tulikubaliana awali.
“Amefanya kazi yake vyema na kutimiza lengo, tunaamini uzoefu wake utatusaidia zaidi msimu ujao kwenye ligi na lengo letu kufanya vyema zaidi,” amesema Ekingo.
Ameongeza kuwa katika ripoti ya kocha amependekeza baadhi ya wachezaji kuachwa na kuongeza wengine jambo ambalo amesema halipingiki na watalifanyia kazi haraka.
“Kila ligi inakuwa na aina ya wachezaji wake, wachezaji wote tuliokuwa nao ni wazuri lakini tunapaswa kuwa na wazuri zaidi kwa ajili ya Ligi Kuu.”
Ekingo amesema wanatarajia kuanza kambi mapema iwezekanavyo kwaajili ya msimu ujao wa ligi na muda sio mrefu mashabiki wao watajulishwa wachezaji gani watakaoachwa na baada ya dirisha la usajili kufunguliwa nao watasajili.