Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKT, Simba vita nzito WPL

Simba Queens 5 2 JKT, Simba vita nzito WPL

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ule utamu wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake (WPL) unazidi kunoga na leo zitashuhudiwa mechi tano za raundi ya nane zikipigwa kwenye viwanja tofauti, huku vinara na watetezi, JKT Queens na Simba wakiendelea na vita yao ya kusaka ubingwa kwa msimu huu na ligi yao binafsi ya hat-trick katika ligi hiyo.

Mechi zitakazopigwa leo ni pamoja na ile ya Simba Queens dhidi ya Fountain Gate Princess itakayopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, Ceasiaa Queens na Alliance Girls Uwanja wa Samora, mjini Iringa, Amani Queens na Bunda Queens zitakazovaana kwenye Uwanja wa Ilulu, mjini Lindi, wakati Yanga Princess na Geita Gold Queens zitamalizana kwenye Uwanja wa Azam Complex na JKT dhidi ya Baobab Queens zitakuwa kwenye Uwanja Meja Jenerali Isamuhyo, vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Wakati mechi zikiendelea huku kwa vigogo kuna ushindani wa timu mbili, JKT Queens na Simba Queens ambao ndio vinara kwenye msimamo.

Ushindani unakuja kwa washambuliaji wa timu zote mbili ambao kwa msimu huu inaonekana kuna vita kali ya kiatu cha dhahabu.

Hadi raundi ya sita wazawa ndio wanaongoza kwenye msimamo wa wafungaji, Asha Mnunka (Simba) na Stumai Abdallah (JKT) wameweka kambani mabao tisa, Winifrida Gerald (JKT) akifunga mabao saba, Asha Djafar (Simba) mabao matano.

Ukiachana na wafungaji, kuna vita ya hat-trick ambako Mkenya Jentrix Shikangwa aliondoka na mpira katika mechi dhidi ya Alliance, Simba iliposhinda mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Mechi saba za WPL mpaka sasa zimezalisha hat-trick sita, mbili zikifungwa na Asha na nyingine Stumai Abdallah, Winifrida Gerald na Amina Ally wa JKT Queens.

Mabao matatu ya Stumai aliifunga Alliance wakati timu yake ilipoondoka na ushindi wa mabao 5-0, Winifrida na Amani mabao yao waliifunga Amani, JKT iliposhinda mabao 10-0 na Mnuka alifunga hat-trick mbili dhidi ya Amani na Ceasiaa.

Kwenye hat- trick zilizofungwa ni Shikangwa pekee ndio nyota wa kigeni aliyefunga mojawapo na zile nyingine tano zote zimefungwa na wazawa ambao wanakimbizana kwenye kiatu cha ufungaji bora.

WENGINE WABADILI

Baada ya mechi tatu za Ligi baadhi ya mashabiki tayari walitabiri timu mbili zilizopanda daraja msimu huu zitashuka mapema pengine zisifike raundi saba.

Imekuwa tofauti baada ya vichapo walivyopata timu za Amani na Bunda Queens zimewazindua usingizini na kuanza kuizoea ligi hiyo kwenye mechi ya tatu kila moja ikifanya vyema.

Hadi raundi ya pili Alliance ilikuwa ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo lakini msimu huu imebadilika kwenye mechi saba imefungwa tano na kushinda mechi mbili.

Kwa sasa Alliance iko nafasi ya tisa kwenye msimamo ikiiachia Ceasiaa iliyopo nafasi ya tatu huku Bunda ikiwa nafasi ya sita na Amani nafasi ya nane.

WAWILI WATEMBEZA VICHAPO TU

JKT ndio timu ya kwanza Ligi Kuu mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote na haijatoa sare ikiruhusu bao moja dhidi ya Yanga Princess iliposhinda mabao 3-1.

Watetezi wametembeza vichapo tu kwenye mechi sita, timu nne Ligi Kuu zimeonja vichapo vikali na timu mbili zikifungwa bao moja moja.

New Content Item (1) New Content Item (1)

Ilianza kutembeza kichapo kwa Bunda cha mabao 4-0, 10-0 dhidi ya Amani Queens, 5-0 Alliance, 3-1 na Yanga huku bao 1-0 wakiwafunga Geita Gold na Fountain Gate Princess.

Simba nayo haijakaa kinyonge licha ya kutoa sare ya bila kufungana na Bunda Queens raundi ya sita ndio timu inayofuata kwa kufunga mabao mengi, ikifunga 23 fofauti ya bao moja na kinara JKT.

Timu hiyo iliifunga Alliance 7-0, Ceasiaa 5-0, Baobab na 5-2 ikimfunga mtani wake Yanga mabao 3-1 na Amani mabao 3-2.

MSIMAMO SASA

Wanajeshi wa kike wanaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi baada ya kukusanya pointi 18 kwenye mechi sita, Simba nafasi ya pili na pointi 16 huku Ceasiaa Queens ikisogea hadi nafasi ya tatu na pointi 13 kwenye mechi saba.

Yanga inasogea hadi nafasi ya nne ikikusanya pointi 12, Fountain Gate Princess nafasi ya tano ikiwa na ponti nane kwenye mechi sita, Bunda Queens imetoka mkiani na kusogea nafasi ya sita ikiwa na pointi nane.

Baobab nafasi ya saba ikiwa na pointi saba kwenye mechi saba, Amani ikilingana pointi na Alliance zote zikiwa nazo sita kwenye mechi saba na Geita ikiburuza mkia kwa kukusanya pointi moja pekee kwenye mechi hizo.

WASIKIE MAKOCHA

Akizungumzia maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Fountain Gate Princess, kocha wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, alisema upungufu wa mchezo uliopita wameufanyia kazi na anaamini watapata pointi tatu japo haitakuwa rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wao.

“Mechi hii tumepata muda mwingi wa kujiandaa kwenye mchezo wetu na Fountain, tunaangalia ubora na udhaifu na tunafanyia kazi ili tupate pointi tatu,” alisema Mgosi.

Kocha wa JKT, Esther Chabruma alisema wachezaji wana morali ya mchezo dhidi ya Baobab Queens na lengo lao ni kupata pointi tatu muhimu nyumbani.

“Hali ya wachezaji iko vizuri, naamini mechi haitakuwa rahisi lakini madhumuni yetu ni kupata pointi tatu muhimu tutapambana ili kuzipata,” alisema Chabruma.

Chanzo: Mwanaspoti