Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKT Queens yaichapa Amani 10-0, Bunda Queens yazinduka

Jkt Queens Kimataifaaaaaa JKT Queens yaichapa Amani 10-0, Bunda Queens yazinduka

Wed, 3 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Moto wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake, JKT Queens hauzimiki kwani licha ya kucheza michezo mitatu mfululizo ugenini lakini timu hiyo imekuwa moto wa kuotea mbali kwa kushusha vichapo na kuendeleza kasi yake ya kuutetea ubingwa wao msimu huu.

Jana ikiwa ugenini mkoani Lindi katika Uwanja wa Ilulu, JKT Queens imeshusha dozi nzito kwa kuichapa Amani Queens mabao 10-0 na kujikita kileleni mwa ligi hiyo huku ikisikilizia matokeo ya watani wa jadi, Simba Queens na Yanga Princess zitakazovaana leo.

Mabao ya JKT katika mchezo huo yamefungwa na Winfrida Gerald ambaye amefunga mabao manne katika dakika ya 20, 44, 47 na 90. Mshambuliaji huyo anafikisha jumla ya mabao sita na kuongoza msimamo wa wafungaji kwenye michuano hiyo.

Mabao mengine yamepachikwa na Amina Bilal aliyefunga mabao matatu katika dakika ya 25, 54 na 57, huku Stumai Abdallah akifunga mabao mawili dakika ya 11 na 63 pamoja na Fatuma Makusanya aliyefunga bao moja dakika ya 17.

Kichapo hicho kizito ni cha pili mfululizo kwa Amani Queens ambayo wiki iliyopita ilikung’utwa mabao 6-1 na Yanga Princess.

Nayo, Fountain Gate Princess ya Dodoma leo imepata ushindi wake wa pili kwenye ligi hiyo kwa kuichapa Alliance Girls bao 1-0 ambalo limefungwa na Amina Ramadhan kwenye mtanange ambao umepigwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Baada ya kuanza vibaya kwa kupoteza michezo miwili nyumbani, Bunda Queens ya Mara leo imezinduka kwa kupata ushindi wake wa kwanza na wa kihistoria katika Ligi hiyo ikiifunga Baobab Queens ya Dodoma mabao 2-1 katika Uwanja wa Jamhuri.

Mabao ya Bunda Queens ambayo ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu, yamefungwa na Hellen Julius na Elizabeth Kihisa. Mchezo wa kwanza Bunda ilichapwa 4-0 na JKT Queens na kupoteza 3-2 dhidi ya Alliance Girls.

Geita Gold imeendelea kuchechemea katika ligi hiyo ikiwa haijaonja ushindi katika michezo mitatu baada ya leo kupoteza mchezo mwingine kwa kufungwa mabao 2-1 na Ceassia ya Iringa katika mtanange ambao umepigwa uwanja wa Samora, Iringa.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mchezo mkali wa dabi ya watani wa jadi, Simba Queens dhidi ya Yanga Princess utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Chanzo: Mwanaspoti