JKT Queens wamebeba ndoo bwana! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya wawakilishi hao wa Tanzania kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa ya Soka la Wanawake kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kuifunga CBE ya Ethiopia kwa penalti 5-4 katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa FTC Njeru, Kampala.
Mbali ya kubeba ubingwa, JKT pia imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Klabu BIngwa Afrika itakayochezwa Ivory Coast mwezi ujao, ikifuata nyayo za Simba Queens iliyobeba taji hilo msimu uliopita na kupata tiketi ya michuano ya CAF na kumaliza kama mshindi wa nne, bingwa akiwa na AS FAR ya Morocco.
Kwa jinsi ilivyocheza tangu ilipotoka kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) ikiivua ubingwa Simba, kinadada hao wa JKT walistahili kabisa kubeba ndoo hiyo katika michuano ya Kampala licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza.JKT ilipangwa Kundi B na na kuanza kugawa dozi dhidi ya AS Kigali, New Generation na Vihiga Queens ya Kenya na kumaliza kama kinara wa kundi kwa kukusanya pointi tisa ikifuatiwa na Wakenya na zote mbili zikienda nusu fainali, huku Kigali na Generation zikiaga michuano.
Katika nusu fainali, JKT ilifanya kweli kwa kuizabua Buja Queens kwa mabao 3-1, iliyomaliza nafasi ya tatu baada ya kuifunga Vihiga katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu kabla ya kupigwa kwa fainali ya wababe hao wa Tanzania na CBE ambao hiyo ilikuwa fainali ya pili baada ya mwaka 2021 kupoteza na Vihiga kubeba ndoo.
Licha ya kupigwa kwenye penalti, CBE iliweka rekodi msimu huu kwa kuwa timu iliyofunga mabao mengi katika michuano hiyo ikitupia kambani mabao 17 na haikupoteza kama ilivyokuwa kwa JKT, japo penalti ziliwapa taji Watanzania baada ya mechi hiyo ya fainali kupigwa dakika 90 za kawaida na 30 za nyongeza.
Katika fainali hiyo kila timu iliingia kwa kutafuta matokeo mazuri na kuandika historia, huku JKT ikiwa imara eneo la mabeki kwa kuizuia C.B.E iliyocheza kwa kasi kusaka mabao na kushuhudia dakika 90 zikiisha 0-0 na hata kwenye dakika 30 za nyongeza hali ilikuwa hiyo hiyo.
Wahabeshi ndani ya dakika 90 ilipata nafasi nyingi za kufunga lakini umakini pamoja na uzuri wa kipa wa JKT, Najiath Idrisa uliipa wakati mgumu safu ya ushambuliaji kupata bao, lakini uzoefu pia ukaibeba wapinzani wao, huku kiungo mkabaji Donisia Minja akionyesha umahiri kuiendesha na kuilinda timu.
Katika penalti, CBE ndio waliokuwa wa kwanza kupiga na kupata kupitia Loza Abela kabla ya Esther Mabanza kusawazisha. Penalti nyingine za JKT zilizowapa taji hilo zilifungwa na Donisia Minja, Winfrida Gerrald, Anastazia Antony na Happyness Mwaipaja aliyefunga ya mwisho. Wengine waliofunga kwa CBE ni Nardos Getenet, Aregash Tedesse na Ebemet ASfawm, huku Mesay Temesgen alikosa.
STUMAI, NAIJAT WANG’ARA
Mbali na kuchukua ubingwa wa mashindano hayo pia straika wa JKT, Stumai Abdallah ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo sawa na kipa Naijat Abbas kubeba tuzo ya kipa bora baada ya kutema mkwaju mmoja wa panalti.
Stumai katika ashindano hayo amekuwa akifanya vizuri na kufunga bao angalau kila mechi huku Naijat akiruhusu mabao matatu tu.
Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Ester Chabruma ‘Lunyamila’ amesema licha ya ushindani walioonyesha Ethiopia, ubora wa kikosi chake umeleta ushindi.
Chabruma alisema mechi ilikuwa ngumu kwasababu wapinzani wao walikuwa na kasi lakini safu yangi ya kiungo ilihakikisha hawatufungi.
“Wachezaji walipambana muda wote lakini Ethiopia nao walikuwa wazuri, wana kasi. Nashukuru maelekezo niliowapa waliyafanyia kazi na hawakuruhusu bao, tunashukuru tumepata ubingwa.” alisema Chabruma.