Kocha msaidizi wa JKT Queens, Azishi Kondo amesema kwa sasa wanakomaa kurekebisha safu ya kiungo na ushambuliaji ili kupata matokeo mazuri mechi ya nusu fainali.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Kampala, Uganda ambako timu hiyo inashiriki michuano ya CECAFA na imetinga nusu fainali na itacheza na kati ya Kampala Queens au CBE.
Alisema katika mechi tatu walizocheza hawakufunga mabao mengi hivyo wako mazoezini kurekebisha mambo madogo hasa eneo la umaliziaji.
Kondo alisema wachezaji wako vizuri na wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ambao watacheza na timu moja kati ya timu hizo.
"Mazoezi tunayotoa tunaona wanayapokea vizuri na wachezaji wako vizuri tunarekebisha maeneo mawili kwa sababu tunahitaji wafunge mabao mengi hasa eneo la ufungaji kwa sababu kwenye mechi zetu tatu tumefunga mabao machache," alisema Kondo.
Kwa upande wa kiungo wa timu hiyo, Donisia Minja alisema pamoja na mazoezi wanayoendelea kufanya lakini kila mchezaji ana ari ya kupambana na kutaka kupewa nafasi.
Minja alisema kila mchezaji akili yake ipo kwenye mchezo wa nusu fainali wako tayari kwa yeyote.