Ndoto za JKT Queens kuwa timu ya pili ya Tanzania kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa wanawake zimeshikiliwa na mchezo wa nusu fainali leo dhidi ya Buja Queens, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Njeru, Uganda kuanzia saa 6:00 mchana.
Wawakilishi hao wa Tanzania katika mashindano hayo ya kuwania kufuzu fainali za Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake kupitia kanda ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), wanaingia katika mechi hiyo ya leo wakipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na kiwango bora walichoonyesha katika hatua ya makundi ambayo walimaliza wakiwa vinara wa kundi B ambalo walishinda mechi zote tatu.
Uimara wa safu ya ulinzi ndio silaha inayoipa jeuri zaidi JKT Queens kwani hadi wanafika nusu fainali, wameruhusu bao moja tu ambalo lilifungwa katika mechi yao ya kwanza dhidi ya AS Kigali waliyoshinda 2-1 na baada ya hapo wakazichapa Vihiga Queens na New Generation kwa bao 1-0 katika kila mechi.
Hapana shaka benchi la ufundi la JKT Queens linaloongozwa na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake Tanzania 'Twiga Stars', Ester Chaburuma litakuwa limefanyia marekebisho safu yao ya ushambuliaji ambayo ilionyesha udhaifu wa kutumia nafasi katika mechi tatu zilizopita za makundi.
Licha ya timu hiyo kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao, washambuliaji wake Stumai Abdalah, Winfrida Gerard na Zainabu Dudu wamekuwa wakishindwa kuzitumia vyema kuipatia timu yao idadi kubwa ya mabao.
Na kuthibitisha hilo, kati ya mabao manne yaliyofungwa na JKT Queens kwenye mashindano hayo hadi sasa, ni moja tu ambalo limepachikwa na mshambuliaji huku mengine yakifungwa na kiungo Donisia Minja na beki Ester Mabanza na moja ni la kujifunga la mchezaji wa wapinzani wao.
Kocha msaidizi wa JKT Queens, Azishi Kondo alisema kuwa wanaingia katika mchezo wa leo wakihitaji ushindi tu na sio vinginevyo.
"Tunawaheshimu wapinzani wetu. Tumewaona ni timu nzuri hivyo hatupaswi kuwadharau. Tumekuja hapa kwa ajili ya kutwaa ubingwa na kupata tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa Afrika na sio matokeo mengine.
"Tumefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mchezo huu wa nusu fainali na tunaamini mwenyezi Mungu atatusaidia tuweze kupata ushindi," alisema Kondo.
Ikumbukwe mwaka jana, Simba Queens walitwaa ubingwa wa mashindano ya Cecafa na kushiriki Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake ambapo walishika nafasi ya nne.