Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKT Queens ishindwe yenyewe Afrika

JKT Queens Vs Abdijan JKT Queens ishindwe yenyewe Afrika

Sat, 11 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Matokeo ya aina mbili katika mechi yake ya leo dhidi ya SC Casablanca ya Morocco kuanzia saa 3 usiku yataibeba JKT Queens na kuipeleka nusu fainali ya Klabu Bingwa wa kwa wanawake Afrika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Laurent Pokou huko Ivory Coast.

Ushindi au sare ya aina yoyote katika mechi ya leo, ni matokeo yatakayoifanya JKT Queens itinge nusu fainali ya mashindano hayo na hivyo kufikia rekodi ya Simba Queens mwaka jana ambapo ilifanikiwa kuwa timu ya Tanzania kufika hatua hiyo.

Ushindi utaifanya kufikisha pointi sita sawa na Mamelodi Sundowns ambayo tayari imeshafuzu kwani pointi hizo hazitoweza kufikiwa na mojawapo kati ya Club Athletic Abidjan na CS Casablanca ambazo kila moja ina pointi moja.

Ikiwa itatoka sare itafuzu na itasonga mbele hata kama Athletic Abidjan itaifunga Mamelodi Sundowns kwani JKT Queens itamaliza na pointi nne sawa na timu hiyo lakini yenyewe itanufaika na matokeo mazuri iliyoyapata katika mechi yake dhidi ya Athletic Abidjan ambapo ilipata ushindi wa mabao 2-1.

JKT Queens inaingia katika mchezo wa leo ikiwakosa wachezaji sita ambao wamerejea Tanzania kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 (Tanzanite Girls) ambacho kesho Jumapili kitakuwa na mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Nigeria kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Katika kundi la wachezaji hao, watano ni wa kikosi cha kwanza na mmoja tu ndiye ambaye amekuwa hapati nafasi jambo ambalo linaweza kuwapa ugumu katik mechi ya leo kama watakuwa hawajajipanga vyema.

Wachezaji sita wa JKT Queens ni kipa Zulfa Makau, mabeki Christer Bahera, Diana Mnally na Violet Nicholaus, kiungo Joyce Lema na mshambuliaji Winfrida Gerard.

Akizungumzia mchezo wa leo, kocha wa JKT Queens, Ester Chaburuma alisema kuwa wamejiandaa kisaikolojia kupata matokeo mazuri katika mechi ya leo ili wafuzu hatua inayofuata.

"Tumekuja hapa Ivory Coast kushindana na sio kushiriki. Malengo yetu ni kutwaa ubingwa ambayo ili yatimie ni lazima tucheze nusu fainali ambayo nayo tunatakiwa tufanye vizuri katika mechi ya kesho (leo) ili tuipate.

"Wapinzani wetu ni timu nzuri lakini na sisi pia ni wazuri na tayari tumeshinda mechi moja hivyo tuna imani kubwa tutafanikiwa kupata ushindi. Tumejiandaa vizuri na wachezaji waliopo wana morali na ari ya kutuwezesha kutupa matokeo mazuri," alisema Chaburuma.

Mechi nyingine ya kundi hilo leo itakuwa ni kati ya Mamelodi Sundowns na wenyeji Athletic Club Abidjan.

Chanzo: Mwanaspoti