Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

JKT Queens inapotufundisha uzalendo kupitia michezo

JKT Queens Players JKT Queens inapotufundisha uzalendo kupitia michezo

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Usiku wa Jumamosi ya Novemba 11, timu ya soka ya wanawake (JKT Queens) inayomilikiwa na jeshi la kujenga taifa (JKT) kupitia klabu ya JKT Tanzania SC ilitolewa hatua ya makundi ya fainali za Klabu Bingwa Afrika nchini Ivory Coast.

JKT Queens ilitolewa baada ya kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Raja Casablanca katika mchezo wa mwisho ambao dada zetu walihitaji sare tu ili kufuzu.

Kutolewa kwenye mashindano siyo kitu kigeni wala cha ajabu, hasa ukizingatia timu hiyo inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo makubwa.

Lakini namna walivyotolewa ndiyo inaweza kufikirisha.

Kwa namna mashindano yalivyokuwa na ubora wa kikosi cha JKT, ni dhahiri kwamba walistahili kusonga mbele.

Lakini kilichowagharimu ni ASILI ya taasisi inayomiliki timu hiyo, JKT.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ni taasisi ya kizalendo na inabidi ionyeshe uzalendo kwa vitendo.

Uzalendo ni mapenzi kwa taifa lako. Kuwa tayari kufa kwa ajili ya taifa.

Hicho ndicho walichokionyesha JKT kama taasisi kupitia timu yao ya JKT Queens.

Kuelekea mchezo huo JKT iliwaruhusu nyota wake sita kurudi Tanzania kwa ajili ya timu ya taifa iliyokuwa icheze na Nigeria Jumapili, Novemba 12.

Wachezaji hao ni kipa Zulfa Makau; mabeki Christer Bahera, Diana Mnally na Violet Nicholaus.

Wengine ni kiungo fundi Joyce Lema na mshambuliaji Winfrida Gerrard.

Hawa ni wachezaji muhimu na tegemeo kwelikweli kwa JKT.

Pata picha una mchezo muhimu wa kufuzu nusu fainali halafu unatoa nyota wako sita wa kikosi cha kwanza unawaruhusu kwa ajili ya timu ya taifa.Ni JKT pekee wanaoweza kufanya hivi.

Na wao wanaongozwa na asili yao, yaani UZALENDO. Kama siyo mzalendo kama JKT huwezi hata kidogo.

ASILI YA JKT NI UZALENDO

Historia ya kuanzishwa JKT inaanzia mwaka 1958 wakati wa ziara ya viongozi wa Taifa wa chama cha kupigania uhuru - Tanu nchini Ghana.

Viongozi hao walikuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na simba wa vita, Rashidi Kawawa.

Viongozi hawa walikwenda Ghana kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya mwaka mmoja wa uhuru wa nchi hiyo.

Itakumbukwa kwamba Ghana ndiyo nchi ya kwanza ya Afrika kupata uhuru, mwaka 1957.

Wakiwa huko, Kawawa alialikwa chakula cha jioni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Golda Meir.

Kawawa alipata fursa ya kuzungumza na kiongozi huyo ambaye alitanabaisha namna taifa la Israel linavyowaandaa vijana wake kutumikia taifa lao kwa moyo wa uzalendo.

‘Simba wa Vita’ alivutiwa na maelezo yaliyotolewa na Meir, namna ya utaratibu unaotumiwa na Israel kuwakusanya na kuwaandaa vijana kijeshi na baadaye kufanya majukumu mengine ya kitaifa kwa ujasiri, uvumilivu, ushirikiano na nidhamu.

Kawawa akamweleza Mwalimu Nyerere juu ya mazungumzo yake na Meir. Nyerere naye akavutiwa na kumwagiza ayafanyie kazi watakaporejea nyumbani.

Waliporejea, Kawawa aliyawasilisha mawazo hayo kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanu, Joseph Kizurira Nyerere, aliyekuwa akisaidiwa na Nangwanda Sijaona.

Viongozi hao waliafiki mawazo hayo na kuyapeleka katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana uliofanyika Tabora Agosti 25, 1958 ili kujadiliwa zaidi na wajumbe.

Hata hivyo, mkutano huo ulishindwa kuidhinisha uanzishwaji wa mafunzo hayo kwa kuwa nchi yetu ilikuwa bado haijapata uhuru.

Lakini baada ya Uhuru wazo hilo liliwasilishwa kwa mara ya pili kwenye Mkutano Mkuu wa Vijana wa Tanu Agosti 25, 1962 mjini Tabora.

Mkutano huo uliazimia kutekeleza wazo la kuanzishwa rasmi kwa taasisi ya kuandaa vijana kuwajengea uzalendo na umoja wa kitaifa.

Baada ya mkutano huo, mapendekezo ya kuanzishwa chombo rasmi cha kitaifa cha kuandaa vijana kuwa wazalendo, yaliwasilishwa serikalini na kuidhinishwa na Baraza la Mawazili ilipofika Aprili 1963.

Serikali iliridhia chombo hicho kiitwe Jeshi la Kujenga Taifa, ndiyo hii JKT iliyopo hadi sasa.

Kwa hiyo ndugu Watanzania, wachambuzi wa soka na mashabiki timu ya JKT Queens, msisikitike sana.

JKT siyo taasisi ya sifa, bali uzalendo. Isingekuwa na maana timu yao ifuzu nusu fainali kwenye mashindano ya Afrika huku timu ya taifa inakosa wachezaji muhimu. Huo siyo msingi wa JKT.

Hongera mwenyekiti Hassan Mabena kwa moyo wa uzalendo na kuishi kwenye misingi ya JKT.

Lakini timu zetu za mitaani zisingekubali hili. Siyo kwamba hazina uzalendo bali misingi ya kuanzishwa kwao ni tofauti na JKT.

Ikitokea siku Simba au Yanga wakawa kwenye mashindano makubwa kama hayo na wana nafasi kama hiyo, mtawalaumu bure.

Malengo yao namba moja siyo uzalendo, bali mafanikio yao.

Wao hawaishi kwa ruzuku ya taifa, wanaishi kwa mafanikio yao ya uwanjani.

Mkiwakwaza uwanjani ni sawa na kuwahukumu kifo.Kwa hiyo kabla hawajafa, watataka ufe kwanza wewe maana wao falsafa yao imejengwa katika mafanikio yao.

Chanzo: Mwanaspoti