Kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa Uwanja wa Samia jijini Arusha ambako kumefanyika juzi baina ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ni ishara tosha kuwa maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 yamepamba moto.
Fainali hizo zitafanyika Tanzania kwa kushirikiana na nchi za Uganda na Kenya.
Ujenzi wa Uwanja huo utagharimu kiasi kinachokadiriwa kufikia Sh286 bilioni, fedha ambazo zinatolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati serikali ikianza maandalizi ya Afcon 2027 kwa upande wa miundombinu, iko haja pia ya kuandaliwa kwa timu bora ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ili iwe na ushiriki mzuri kwenye mashindano hayo na ifike mbali badala ya kugeukwa msindikizaji.
Hakutakuwa na sababu wala maana ya kuandaa fainali hizo ambazo ni mashindano yenye hadhi na thamani kubwa zaidi ya soka barani Afrika huku tukiwa hatuna timu imara ya taifa ambayo itaishia hatua za awali na kubaki kutazama mechi za wenzetu kwenye hatua zinazofuata.
Mapendekezo mengi ya namna ya kujenga timu bora na shindani ya taifa kwa ajili ya Afcon 2027 yamekuwa yakiwalenga zaidi kutafuta na kutumia idadi kubwa ya wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya na kwingineko duniani.
Changamoto kubwa ambayo inaonekana ni kikwazo katika utafutaji wa hao wachezaji wenye asili ya Tanzania ni kutokuwepo kwa sheria ya kuruhusu uraia pacha ingawa serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa ufafanuzi kuwa ipo sheria ya kuruhusu uraia wa hadhi maalum ili nchi iweze kunufaika na wataalam au vipaji vyenye asili ya Tanzania ambavyo tayari vina uraia wa nchi nyingine.
Lakini ukiondoa hiyo, nyingine ni kutokuwepo kwa idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza ligi za madaraja ya juu ambao wana asili ya Tanzania na kundi kubwa ni wale wanaocheza katika madaraja ya ligi yasiyo na ushindani mkubwa na ubora wa kuifanya Taifa Stars iwe tishio kwenye soka la Afrika.
Katika fainali zilizopita za Afcon, Tanzania ilikuwa na wachezaji sita wenye asili ya Tanzania ambao walikuwemo kikosini na kati ya hao ni mmoja tu, Charles M’Mombwa ambaye anacheza ligi ya daraja la juu ambayo ni Ligi Kuu ya Australia katika timu ya McArthur lakini wengine watano wote wanacheza timu za madaraja ya chini.
Ipo njia mbadala ya kupita kama ile ya kutegemea wachezaji wenye asili ya Tanzania inaonekana inachelewa kuleta matunda kwa haraka nayo ni kushawishi nyota wa kigeni wenye ubora wa hali ya juu kwenye ligi yetu wabadili uraia na kuridhia kuitumikia Taifa Stars.
Hawa ni wale wachezaji ambao kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wachezaji mahiri na bora katika mataifa yao, wana uwezekano mdogo na pengine hawawezi kuwemo au kujumuishwa katika vikosi vya timu zao za taifa kwenye mechi za kimashindano.
KANUNI ZINARUHUSU
Kwa mujibu wa kanuni za uraia na uwakilishi wa wachezaji katika timu za taifa, mchezaji anaweza kuitumikia timu ya taifa ikiwa atakuwa raia wa kuzaliwa wa nchi husika au atakuwa na uraia wa kuomba.
Kanuni hizo zimesisitiza kuwa kwa mchezaji ambaye anatumikia taifa ambalo sio la asili au hajazaliwa hapo, anapaswa kufanya uamuzi huo pasipo kulazimishwa au kupewa fedha lakini iwe kwa utashi wake tu.
Mfano wa hilo tunaweza kuuona kwa mshambuliaji Bernard Kamungo ambaye hana asili ya Marekani kwa kuzaliwa wala wazazi wake lakini ameshawishika kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo kwa kile kinachoonekana ni hamu ya kufanikiwa na kushiriki mashindano makubwa zaidi kama Kombe la Dunia.
Mwongozo huo wa Fifa umesisitiza kuwa nyaraka muhimu ya uthibitisho inapaswa kuwa hati yake ya kusafiria (pasipoti).
Mchezaji huyo kama yupo zaidi ya umri wa miaka 18, anapaswa kuwa ameishi katika nchi husika kwa muda usiopungua miaka mitano.
Mchezaji husika anapaswa asiwe amecheza mechi yoyote ya kimashindano kwa timu ya taifa jingine ingawa kwa mechi za kirafiki inaruhusiwa. Ikumbukwe kitendo cha kuwemo katika orodha ya mechi ya kimashindano, kinatosha kumfanya mchezaji akose uhalali wa kikanuni kutumikia taifa jingine.
Hii inamaanishwa kwamba mchezaji kama Kipre Junior wa Azam FC anaweza kuichezea Taifa Stars kama atashawishiwa na kubadili uraia kwa vile hadi itakapofika Afcon 2027, atakuwa ametimiza miaka mitano ndani ya ardhi ya Tanzania.
UJANJA KUPITIA VIJANA
Kanuni hiyo ya uraia na uwakilishi kwa timu za taifa, inafafanua kwamba ili mchezaji ambaye hana asili ya taifa fulani apate hadhi ya kulitumikia akiwa na umri chini ya miaka 18, anapaswa awe ameishi kwenye hiyo nchi kwa muda usiopungua miaka mitatu.
Kunaweza kutengenezwa kanuni ya kuruhusu timu za vijana kuwa na wachezaji wa kigeni wenye umri chini ya miaka 18 ili kupata wale wanaoonekana wanaweza kuwa na msaada kwa Taifa Stars kwenye Afcon 2027 na kisha kuwashawishi waichezee siku za usoni.
Mfano Yanga ikiwa na wachezaji wanne, Simba ikawa na idadi kama hiyo sawa na Azam FC kwenye vikosi vyao vya vijana, maana yake kutakuwepo na wachezaji 12 wanaoweza kuongeza wigo kwa benchi la ufundi la Taifa Stars.
Kanuni hiyo ikianza kutumika katika msimu ujao, maana yake hadi itakapofika 2027, wachezaji hao watakuwa wameshatimiza takwa la kikanuni maana watakuwa wameishi nchini kwa muda usiopungua miaka mitatu.
MIFANO IKO HAI
Zipo nchi nyingi barani Afrika na hata Ulaya ambazo zimewahi kunufaika na wachezaji ambao hawajazaliwa na wala hawana asili ya mataifa husika lakini zikawatumia katika timu zao za taifa.
Kipa aliyeichezea Ivory Coast kwenye Afcon mwaka huu Charles Folly Ayayi ni mzaliwa wa Togo na wazazi wake wanatoka nchini humo lakini akachagua kutumikia taifa ambalo sio la asili yake kwa vile ameishi kwa muda mrefu.
Kiungo wa timu ya taifa ya Burkina Faso, Blati Tour kiasili ni wa Ivory Coast kama ilivyo kwa Stephane Aziz Ki.
Nyota wa zamani wa Chelsea na Atletico Madrid, Diego Costa aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Hispania huku yeye na wazazi wake wakiwa wamezaliwa Brazil.
Mshambuliaji wa zamani wa Benfica, Rogelio Funes Mori alizaliwa na kukulia Argentina ambako hata wazazi wake ni wa huko na aliwahi hata kuzitumikia timu za taifa za vijana za taifa hilo lakini baadaye akabadili uraia na kuichezea timu ya taifa ya Mexico.
Hivi karibuni, mchezaji Mohamed Diomande aliyezaliwa na kukulia Ivory Coast hadi kuzichezea timu za taifa za vijana za nchi hiyo, aliamua kubadili uraia na sasa anaitumikia timu ya taifa ya Ghana.