Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Issa Abushehe: Messi wa Bongo aliyecheza Misri bila mshahara

Issa Abushehe Issa Abushehe

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Septemba 19, 2022 ilikuwa ni siku nzuri kwa kiungo mshambuliaji, Issa Abushehe ‘Messi’ baada ya kupata dili la kujiunga na Al Mokawloon Al Arab inayoshiriki Ligi Kuu Misri akitokea Coastal Union ya Tanga.

Hata hivyo, baada ya dili kukamilika, huku wadau wa soka nchini wakimtabiria makubwa kutokana na uwezo alionao, ghafla msimu huu amerudi tena na kujiunga na Biashara United ya Mara iliyopo Ligi ya Championship.

Kurudi kwa nyota huyo kumelifanya Mwanaspoti kumtafuta, ili kujua kilichomrudisha nyumbani naye akafunguka mengi. Endelea naye...!

SAFARI YA MISRI

Abushehe anasema baada ya kudumu kwa misimu minne Coastal ndipo ilikuja ofa ya kwenda Misri kwa ajili ya majaribio.

“Meneja wangu (Jamal Kajia) aliniambia Al Mokawloon inanihitaji na kama nitafanya vizuri katika majaribio basi watanisajili, nashukuru baada ya kufika kule nilifaulu na wakanisajili moja kwa moja, japo sikucheza,” anasema na kuongeza;

“Sikucheza kwa sababu wakati natoka Tanzania nilikuwa na jeraha la goti hivyo nilijitonesha na nilipofanyiwa vipimo nikatakiwa kufanyiwa upasuaji na nikatakiwa nikaa nje kwa miezi tisa na maisha yangu yakaanza kubadilika kuanzia hapo.”

AONDOLEWA USAJILI

Abushehe kwa majeraha hayo aliondolewa katika mfumo wa usajili wa klabu hiyo na Chama cha soka Misri (EFA) ndipo alipoona ndoto za kucheza huko zinafikia ukingoni, kwani asingeweza kurudi kwenye ushindani kwa haraka zaidi.

“Mkataba wangu ulikuwa wa miaka mitatu na niliumia msimu wa kwanza, ndipo viongozi wakaniambia wananiondoa kwani ingekuwa ngumu kucheza ila watanitibia hadi nitakapopona, kiukweli nilikubaliana na matakwa yao waliyoniambia,” anasema.

HALIPWI MSHAHARA

Nyota huyo anasema kwa muda wote aliokuwa Misri na klabu hiyo hakuwa analipwa mshahara isipokuwa alichokuwa anapata ni posho tu.

“Tangu nimefika nilikuwa silipwi mshahara kama wachezaji wenzangu kwani niliingia kipindi kibaya cha majeraha, hivyo niliambulia posho tu japo haikuweza kuniumiza sana kwa vile huduma zote za matibabu walinigharamia.”

AOMBA KUSEPA MISRI

Anasema baada ya kudumu kwa msimu mmoja aliomba kuondoka ili kutafuta timu ya daraja la chini itakayoweza kumrudisha katika ushindani.

“Licha ya mkataba wangu kubakia miaka miwili, ila ulikuwa unaniruhusu kuondoka pindi nitakapopata timu nyingine. Niliona ni vyema kuondoka kwa vile nisingeweza kuingia tena kikosi cha kwanza kwa haraka kama mwanzoni.

“Wenzangu walikuwa tayari wameshachanganya hivyo, nilihitaji timu ya daraja la chini ili nianze kujitafuta upya na nashukuru walinielewa, ndipo niliamua kujiunga na Biashara United ambayo haina presha zaidi kwangu.”

LIGI MISRI SI MCHEZO

Abushehe anasema, ipo tofauti kubwa kati ya soka la Tanzania na Misri kwani wenzao wapo siriazi zaidi tofauti na sisi.

“Wenzetu wanajua wanachokifanya kuanzia wachezaji, viongozi na hata mashabiki ndio maana unaona hata katika michuano ya nje wanafanya vizuri, kikubwa nilichokiona jamaa wanafanikiwa kwa kupenda wanachokifanya,” anasema na kuongeza;

“Jambo lingine wanazingatia masharti wanayopewa kwa mfano unapotakiwa kufika mazoezini muda fulani, lazima uwepo na ukichelewa unakatwa hadi mshahara, hilo linawaongezea umakini tofauti na ninavyoona huku.”

KUFELI NJE

Anasema yapo mambo mengi yanayowafelisha wachezaji wengi wanapoenda kucheza nje japo Watanzania hawataki kuamini katika ukweli.

“Mimi nipo hapa, lakini nimesikia maneno mengi yakizungumzwa juu yangu, eti nimefeli mara kiwango kimeshuka ila niliamua kukaa kimya. Kila mmoja ana changamoto zake anazopitia hivyo ni bora ukasikiliza kuliko kuongea yale usiyoyajua.”

BONGO ANAPITA TU

Anasema kucheza Biashara Utd ni moja ya njia ya kurudi katika ubora na sio kama ameshafika, kwa kuwa malengo ni kucheza nje ya nchi.

“Kucheza hapa haina maana nimefika au nimefeli isipokuwa ninapita tu, kwanmalengo ya nje yapo na uzuri mkataba wangu ni wa mwaka mmoja, hivyo utakapoisha nitaamua timu nyingine ya kwenda kwani ofa bado zipo nyingi.”

NJE YA SOKA

Nyota huyo anasema kama asingekuwa mchezaji basi angekuwa msanii wa kizazi kipya kwani uwezo wa kuimba na kutunga nyimbo mbalimbali anao.

“Napenda sana kuimba japo sijawahi kurekodi nyimbo yoyote, kwangu ni kipaji kingine nilichojaaliwa na kwa wanaonijua wanatambua nina uwezo huo, mwanzoni nilikuwa naimba sana ila nilivyojikita katikae mpira nikaacha,” anasema na kuongeza;

“Mbali na kuimba ila mimi pia ni mfanyabiashara, kuna biashara zangu ndogondogo nisingependa kuziweka wazi nazifanya, huko mbeleni baada ya kustaafu soka nataka nijikite katika kazi hiyo kwani ni miongoni mwake ninazozipenda kuzifanya.”

MECHI ASIYOISAHAU

Anasema moja ya mechi ambayo hatokaa akaisahau maishani mwake ni ile ya Coastal Union iliyokuwa inapambania kupanda Ligi Kuu Bara.

“Nakumbuka mechi ya mwisho ya Coastal na Mawenzi Market iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro mwaka 2018, kiukweli sitaisahau kwa sababu ilikuwa ni ngumu na tulihitaji kupata ushindi tu ili tupande Ligi Kuu,” anasema na kuongeza;

“Hiyo mechi ilikuwa ya Kundi ‘B’, ila nashukuru tulishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Raizin Hafidh na Athuman Iddi ‘Chuji’ ila ugumu wake ulitokana na ugeni wetu kule kwao, lakini tulirushiwa mawe uwanjani hivyo sitalisahau hilo.”

SALUTI KWA MGUNDA

Watu ambao hatowasahau nyota huyo ni waliokuwa makocha wa Coastal Union, Juma Mgunda, Joseph Lazaro na kocha wa makipa, Salim Wazir.

“Coastal nilijiunga nayo kupitia timu ya vijana ila Juma (Mgunda) aliponiona akaniambia wewe huku utacheza ila kiwango ulichokuwa nacho utachezea wakubwa, kiukweli alinipa nafasi hiyo na sitokaa nikamsahau katika maisha yangu,” anasema.

MALENGO YA SASA

Anasema moja ya malengo yake kwa sasa ni kuipigania timu ya Biashara United anayoichezea msimu huu ili ipande Ligi Kuu Bara.

“Tuna michezo michache iliyobakia na ukiangalia nafasi tuliyopo sio mbaya japo tunahitaji kupambana zaidi kwa sababu nimeletwa hapa kutokana na uzoefu wangu hivyo viongozi na mashabiki wana matumaini na mimi ya kutimiza malengo hayo.”

Chanzo: Mwanaspoti