Mwenyekiti wa zamani wa Simba SC Ismail Aden Rage ameshauri Katiba ya Klabu hiyo inapaswa kufanyiwa marekebisho ili kuleta usawa wa umiliki kati ya Wanachama na Mwekezaji.
Simba SC imekuwa kwenye mchakato wa mabadiliko ya kiutendaji, huku Wanachama wakipewa nguvu ya kikatiba kumiliki Asilimia 51 ya hisa na Mwekezaji akipewa Asilimia 49.
Rage amesema kutokana na muongozo wa umiki wa hisa, Katiba ya Simba SC inapaswa kufanyiwa marekebisho na kuwapa Wanachama wenye asilimia kubwa kuwa na sauti ya mtu atakaewasemea kwenye Bodi ya Wakurugenzi.
Amesema kwa maoni yake binafsi angependa kuona Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC akitoka upande wa Wanachama, ambao wana kila sababu ya kuwa na mtu huyo kutokana na umiliki hisa zao.
Rage akaenda mbali zaidi kwa kusema, Mwenyekiti wa Bodi anapaswa kuwa Rais wa Simba, hivyo amehimiza Wanachama kulitazama hilo ambalo linapaswa kupewa nguvu kikatiba.
“Ukweli uko pale pale kuna maeneo ya Katiba lazima yafanyiwe marekebisho, mfano wanasema Wanachama wa Simba SC asilimia yao ni 51% na Mwekezaji ni 49%, ifike wakati irekebishwe Mwenyekiti wa Bodi awe Rais wa Simba, kwa sababu sisi ndio tuna Share kubwa (51%)”
“Kuna msemo wanasema Mimi siuelewi kabisa , wanasema Wanachama tununue hisa! kwa nini tunnunue hisa? sisi tumeitengeneza Klabu tangu 1936, ndio maana Wawekezaji wakaja Simba SC kwa sababu tuna Fan Base kubwa (Mashabiki wengi) na nimefurahi Shabiki mmoja amesema nguvu ya Simba SC ni Wanachama na Mashabiki wao” amesema Rage
Simba SC juzi Jumapili (Januari 29) ilifanya Uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti iliyokuwa inawaniwa na Murtaz Mangungu na Moses Kaluwa, huku Wagombea nafasi ya ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi walikuwa 12.
Katika uchaguzi huo ambao matokeo yake yalitangazwa jana Jumatatu (Januari 30) Alfajiri, Moses Kaluwa alipata kura 1,045 huku Mangungu ambaye alikuwa anatetea kiti chake akipata jumla ya kura 1,311.
Kwa upande wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi walioshinda ni Dr Seif Ramadhan Muba (1636), Asha Baraka (1564), CPA Issa Masoud Iddi (1285), Rodney Chiduo (1267) na Seleman Harubu (1250).
Jumla ya Wanachama Simba SC waliopiga Kura ni 2363 Kura halali, lakini Kura halali zilikuwa 2356.