BODI ya Ligi Tanzania (TPLB), imezikumbusha timu za Ligi Kuu Bara kwamba kanuni ya kuwachezesha wachezaji 12 kwenye mechi moja, ililenga michuano ya kimataifa pekee na si vinginevyo.
Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo aliiambia Mwanaspoti juzi, wanazikumbusha utaratibu wa kuchezesha wachezaji wanane kwenye Ligi Kuu kwamba hautabadilika badala yake timu zinapaswa kujipanga zenyewe katika matumizi ya mastaa wao.
Kasongo alisema kwenye michuano ya CAF ilikuwa juu ya klabu hizo kuwatumia wachezaji hao kama wanavyotaka, ila kwa ligi ya ndani zinapaswa kuzingatia muongozo wa kanuni hizo.
“Timu zenyewe hasa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa ndizo zilitushinikiza kuongeza idadi hiyo ili kuweza kufanya vizuri kimataifa kutokana na wachezaji wetu wa ndani wengi hawana uzoefu na ubora wa kutoa ushindani kwenye michezo ya kimataifa ambayo ina ushindani,” alisema na kuongeza;
“Napongeza mwanzo sio mbaya wageni waliosajiliwa wameweza kutubeba kimataifa na kufanikiwa kupata nafasi nne za kuiwakilisha nchi kimataifa lakini hilo lisiwe sababu ya kutushawishi tuongeze idadi ya wageni kwenye ligi yetu, haiwezekani na haitatokea, wazawa na wao wanahitaji kukuzwa na kujengewa uzoefu.
“Hatuwezi kuendelea kusikiliza kila kitu tunachoshauriwa. Kwenye kanuni hii tulipokuwa tunaipitisha tulishirikisha viongozi wa klabu na kukubaliana. Hakuna haja ya kushindwa kupandisha vipaji vya wazawa kwasababu ndio wanaoiwakilisha nchi kwenye timu ya taifa.”
Kasongo alisema kama wanaona gharama kusajili nyota wengi ambao hawawatumii waangalie bajeti zao na wafanye kile kinachoweza kuwabeba, lengo ni moja tu kwamba wanatakiwa kuwapa vipaumbele na wazawa ili wakuze vipaji kwasababu wageni wanaokuja hapa hawawezi kuiwakilisha Taifa Stars.
“Mimi nashauri gharama za kusajili waanzishe vituo vya vipaji,” alisema.