Klabu ya Simba imeendelea kushuka majembe mapya baada ya kutambulisha yule winga aliyeripotiwa mapema juzi kwamba ameshasaini mkataba wa miaka miwili, Aubin Kramo Kouame kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast, huku koch wa timu hiyo akitua nchi jana.
Simba ilimtangaza winga huyo anayemudu kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani na anayekumbukwa kwa kumpindua beki Joash Onyango kwenye mechi ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na msimu uliopita alikiwasha kwenye michuano hiyo wakifika nusu fainali.
Mabosi wa Simba ilimfuata Kramo kimyakimya na kumpa mkataba wa miaka miwili akiwa kwao kabla ya kumleta fasta na jana kumtambulisha saa 7 mchana akiwa mchezaji mpya wa pili kuweka hadharani na klabu hiyo.
Winga huyo anayemudu kutumia miguu yote miwili kwa ufasaha, aliidhuru Simba kwenye mechi hizo za makundi akihusika kwenye mabao mawili ya Asec, mechi ya kwanza ya hapa jijini Dar es Salaam ndiye aliyemsababishia balaa beki Joash Onyango akizuia pasi ya Mkenya huyo kisha mpira kuunasa Stephanie Aziz KI aliyewapunguza mabeki wa wekundu hao kisha kwenda kumfunga kipa Aishi Manula wakisawazisha bao licha ya pambano kuisha kwa Asec kulala mabao 3-1.
Walipoenda kurudiana Machi mwaka jana, alifunga bao la kuongoza dakika ya 17 baada ya kuizidi akili mabeki wa wekundu hao waliolala ugenini mabao 3-0 na kwa hasira mabosi wa Simba kumpandia ndege, ili kumalizana naye aje kuvaa uzi wa rangi nyekundu na nyeupe.
Usajili wa winga huyo unamaanisha kwa sasa Simba imepata mtu muafaka katika kushambulia kutoka pembeni akiwa sambamba na Leandre Willy Onana aliyetambulishwa juzi ambaye sifa zake zinafanana na alizonazo Muaivory Coast huyo.
Hiyo itamrahisishia kazi kocha Robertinho aliyerejea nchini juzi kutoka Brazili aliyetaka kuletewa winga anayejua kazi ikiwa ni mapendekezo yake.
Aubin mwenye miaka 27 alijiunga na Asec mwaka juzi akitokea FC San Pedro pia aliwahi kukipiga Africa Sports iliyomsajili akitokea Asec aliyoichezea hapo mwaka 2015.
Mbali na Onana na Aubin, Simba pia inahusishwa kumsainisha beki wa kati kutoka Cameroon, Che Fondoh Malone JR wa CotonSport pamoja na kipa Caique Luiz Santos atakayetua nchini kesho ambao wanaweza kutambulishwa kuanzia wikiendi hii kabla ya timu kwenda Uturuki Jumanne ijayo.
Kambi hiyo itakuwa ya wiki tatu ya kujiandaa na msimu mpya, huku asilimia kubwa ya wachezaji wote wakiwa wameshafanyiwa vipimo vya afya na kufanmyiwa taratibu za kuondoka, japo Habib Kyombo na Joash Onyango wakitolewa kwa mkopo Singida Big Stars.
Onyango aliyepo Kenya kwa sasa, aliomba kuondoka lakini viongozi walikuwa wasikilizia dili la Che Fondoh Malone ili kuja kuziba nafasi yake aungae na Kennedy Juma na Henock Inonga, wakati Kyombo ana mkataba mrefu na kabla ya kuichezea Simba aliwahi kusajiliwa na Singida msimu uliopita sambamba na Yanga na uongozi wa Simba uliomba uachiwe na sasa inamrejesha kiaina.