Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ishu ya jezi Yanga, Mamelodi ilivyo

Jezi Mame Yanga Ishu ya jezi Yanga, Mamelodi ilivyo

Tue, 26 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baadhi ya wadau wa soka nchini wameanza kuwa na hofu juu ya namna itakavyokuwa katika matumizi ya jezi kwa timu za Yanga na Mamelodi Sundowns wikiendi hii katika mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na miamba hiyo rangi zao mama kufanana.

Ni kweli kuwa Yanga ya Tanzania na Mamelodi ya Afrika Kusini zote zinatumia rangi za kijani na njano kama utambulisho mama hata bluu na nyeusi.

Itakuwaje? Kwa mujibu wa taratibu, mara nyingi mwenyeji ambaye ni Yanga atapata kipaumbele cha kuwa wa kwanza kuchagua jezi gani ambazo atataka kuzitumia na mara nyingi Wananchi wamekuwa wakitumia jezi zao chaguo la kwanza za njano na muda mwingine hutumia chaguo la tatu ambazo ni nyeusi na kuna kipindi zilikuwa zikionekana kuwa na bahati.

Hivyo kama Yanga ikitumia jezi za njano, basi Mamelodi itabidi kutumia jezi zao chaguo la pili ambao ni bluu, huku chini zikiwa na bukta nyeupe na kama Wananchi wataamua kwenda na jezi zao za bahati ambazo ni nyeusi, Masandawana wanaweza hata kuvaa uzi chaguo la kwanza ambao juu ni njano na chini bukta za bluu.

Lakini pia Yanga inaweza kuamua kuvaa jezi chaguo la pili ambazo ni kijani, hizo haziwezi kuathiri machaguo ya kwanza na pili ya jezi kwa Mamelodi ambao wanatarajiwa kutua nchini kesho, Jumatano, kwa ajili ya mchezo huo.

Mgongano wa jezi kati ya Yanga na Mamelodi hauwezi kutokea kwani mara nyingi kabla ya timu kukabiliana huwa kuwa kikao cha maandalizi ya mchezo (pre match meeting) ambacho mbali na mazungumzo mengine hubainisha jezi ambazo zitatumiwa na kila upande, hivyo huzingatia kutowepo kwa mgongano.

Hivi karibuni nchini England mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake kati ya Arsenal na Chelsea ililazimika kuchelewa kuanza kwa takriban dakika 30 kwa sababu timu zote mbili zilikuwa zimevaa soksi zinazofanana, jambo ambalo ni kinyume na kanuni.

Timu hizo ziliingia uwanjani kupasha misuli moto zote zikiwa zimevaa soksi nyeupe na baada ya mwamuzi kuingilia kati ililazimika Arsenal kununua soksi za rangi tofauti kwenye duka la Chelsea maana ilikuwa timu ngeni.

Arsenal ililazimika kuficha kwa gundi nembo za Chelsea na mtengenezaji wa vifaa kampuni ya Nike kwa sababu za kibiashara na kimkataba.

Chanzo: Mwanaspoti