Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Yacouba Songne amefunguka kinachomfanya asionekane kwenye timu yake mpya ya Ihefu FC kuwa ni kutokana na kukosa kibali cha kazi.
Yacouba alitua Ihefu kupitia dirisha dogo sambamba na viungo wawili kutoka Simba waliochukuliwa kwa mkopo, Nelson Okwa na Victor Akpan, hajaonekana kabisa uwanjani tangu atambulishwe mwishoni mwa mwezi uliopita.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, nyota huyo kutoka Burkina Faso, alisema yupo tayari kuitumikia timu hiyo huku akithibitisha anatamani kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wataipambania timu hiyo kubaki msimu huu.
ALSO READ
Huko Bara kuna vita ya nduguSoka Feb 11 2023
“Nafanya mazoezi na timu na niko fiti kinachoniweka nje ni suala la kibali, lakini sio uwezo kama inavyozungumzwa nje ya uwanja, bahati nzuri uongozi umeniahidi kulifanyia kazi hilo kabla ya ligi kumalizika huenda nikacheza mechi inayofuata,” alisema Yacouba aliyeifungia Yanga mabao manane msimu wa 2020-2021 kabla ya kuumia na kuwa nje msimu uliopita.
“Nimetoka nje ya uwanja nikijiuguza majeraha natamani kutumia nafasi hii niliyonayo sasa kwa kucheza lakini changamoto iliyopo ipo nje ya uwezo wangu nimewaachia viongozi wafanyie kazi ili na mimi niendelee na majukumu yangu.”
Katibu Mkuu wa Ihefu, Zagalo Chalamila alipotafutwa na Mwanaspoti alithibitisha suala hilo kuwa wapo kwenye mchakato wa kulikamilisha kwani tayari wamelipia na muda wowote kuanzia sasa mchezaji huyo ataanza kuitumikia timu hiyo.
“Ni kweli lakini tupo kwenye mchakato wa kukamilisha kesho (leo) jioni tutakuwa na kitu cha kuzungumza kwa usahihi zaidi kuhusuana na suala hilo,” alisema Chalamila.