MARA baada ya Simba kuanza harakati za ujenzi wa uwanja mpya kwa kuanzisha rasmi mchango kwa ajili ya uwanja huo, uongozi wa Yanga ni kama umejibu mapigo kwa watani zao mara baada ya kuweka wazi mipango yao ya ujenzi wa uwanja.
Simba tayari wameshaweka hadharani mchakato wa uchangiaji wa ujenzi wa uwanja huo kupitia sehemu mbalimbali jambo ambalo limeibua gumzo nchini ambapo tayari wapenzi na wanachama wake wameshaanza kuichangia timu yao.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha Masingiza aliweka wazi kuwa mradi wao wa ujenzi wa uwanja ambao unafahamika kwa jina la Kigamboni Complex ‘Home of Champions’ tayari umeshawapata wakandarasi ambao wataanza kazi muda wowote kuanzia sasa.
“Mradi tayari ulishapata wakandarasi wa kuuanza kufanya kazi ambapo muda wowote kuanzia sasa Kigamboni Complex Hom of Champions itaanza kufanyiwa kazi jambo ambalo ni maendeleo makubwa kwa klabu yetu.
“Yanga tuna mipango mingi sana endelevu na bora kwa ajili ya klabu hivyo kuna vitu vingi sana vinatakiwa kukamilika ili watu waone maendeleo yenyewe,”alisema kiongozi huyo.