Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ishu ya Saido, Chama, Mabosi Simba waanika kila kitu

Chama Saido Mlk Ishu ya Saido, Chama, Mabosi Simba waanika kila kitu

Fri, 19 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Viungo nyota wa Simba, Saido Ntibazonkiza na Clatous Chama wote kwa sasa hawapo nchini, mmoja akiwa kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 na mwingine ameenda mapumziko, huku hatma yao ndani ya klabu wakiwa hawaijui, hata hivyo ni kwamba mabosi wa Simba wamemaliza kazi.

Chama aliyeondoka nchini akiwa amesimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kosa la utovu wa nidhamu yupo Afcon akiiwakilisha Zambia iliyopo kundi moja na Tanzania, Morocco na Dr Congo, wakati Saido ameenda Burundi bila kuafikiana na mabosi juu ya dili la kuongeza mkataba mpya.

Hata hivyo, taarifa kutoka Simba ni kwamba wachezaji wamebakishwa kikosini hadi mwishoni mwa msimu, huku Aubin Kramo akichomolewa jumla kwenye usajili wa timu hiyo kama tulivowadokeza katika gazeti la jana.

Tuanze na Saido. Kiungo huyo wa zamani wa Vital’O ya Burundi, Yanga na Geita Gold aliondoka juzi kwenda Burundi kwa mapumziko mafupi, huku akiwa hajaafikiana na viongozi hao kusaini mkataba mpya, ambapo awali ilielezwa alikuwa apigwe panga sambamba na Moses Phiri na Chama kabla ya upepo kumgeukia Jean Baleke aliyeondolewa klabu na Mzambia Phiri, kisha Kramo akafuata dakika za mwishoni.

Inaelezwa, vigogo wa Simba wameshitukia jambo kwa wawili hao na kuwataka kurudi nchini haraka pale kila mmoja atakapomaliza ratiba zake ili wamalizane kimkakati na kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwishoni mwa msimu.

Mwanaspoti kupitia vyanzo vyake mbalimbali limethibitisha Saido hadi anaondoka alikuwa hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kuwepo Simba kutokana na kutofautiana katika maeneo tofauti ikiwemo, uhitaji, maslahi na muda wa mkataba.

Staa huyo aliyeibuka mfungaji bora msimu uliopita akitupia mabao 17 sawa na Fiston Mayele aliyekuwa Yanga kabla ya kuuzwa Pyramids ya Misri, anataka mkataba mpya wa mwaka mmoja na nusu na kuendelea huku Simba  ikilenga kumpa mkataba mfupi jambo ambalo bado linajadiliwa na pande zote mbili.

“Tunaendelea kufanya mazungumzo ya pamoja baina ya pande zote mbili na tukipata mwafaka tutawapa majibu. Baada ya mapumziko Saido atarudi nchini ili tulimalize hili na naamini ataendelea kuwa mchezaji wetu,” kilisema chanzo kutoka Simba na alipotafutwa Saido alikiri kuwepo mapumziko Burundi na kusema hawezi kulizungumzia jambo hilo huku akisema; “Nitarudi Tanzania siku si nyingi.”

Kwa upande wa Chama baada ya vikao vya kwanza baina yake na uongozi wa Simba ambavyo vilifanyika kwa njia ya mtandao na kutofikia mwafaka, ametumiwa barua pepe (email), akitakiwa kurudi nchini haraka tu mara baada ya timu yake ya taifa kufikia ukomo wa ushiriki wa Afcon mwaka huu ili wamalize jambo hilo.

“Chama hatuna shida naye kubwa kwani sisi ndio tulimsimamisha, lakini hata hivyo tumemtumia ujumbe wa kumtaka arudi nchini mara moja pale ambapo timu yake itamaliza mashindano.

Hatufanyi hivyo bila sababu, unajua kwa sasa timu ina wachezaji wapya na kocha bado hajatengeneza kikosi kamili hivyo tunataka kabla ya mashindano ya klabu kuendelea, tuwe tayari na wachezaji wetu na timu imara,” kilieleza chanzo hicho.

Saido anatarajiwa kurejea nchini kuanzia Jumatano ya ijayo, huku Chama akisikilizia Zambia itafikia wapi kwenyue fainali hizo za Afcon 2023 zinazofanyikia Ivory Coast.

Kubakizwa kwa Chama na Saido, kunaifanya Simba iendelee kuimarika hasa baada ya kusajiliwa kwa nyota wengine wapya akiwamo Salehe Karabaka, Ladack Chasambi, Edwin Balua, Pa Omar Jobe na Freddy Michael Kouablan ambao wanacheza eneo la ushambuliaji, sambamba na kiungo mkabaji Babacar Sarr.

MSIKIE KAJULA Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alipotafutwa jana alitoa ufafanuzi wa nyota hao watatu yaani Chama, Saido na Kramo ili kuwatoa wasiwasi mashabiki wa Simba kutokana na kuwepo kwa taarifa tofauti.

Kajula alisema nyota hao wote ni wachezaji halali wa Simba huku kila mmoja akimwelezea sababu za uwepo wake ndani ya klabu hiyo.

“Kramo bado hajapona vizuri ila anaendelea kuimarika, mchezaji anapotoka kwenye majeraha hawezi kuanza kucheza moja kwa moja. Tulichokifanya Kramo ni kumuondoa kwenye mfumo wa TFF, lakini ni mchezaji wetu, tunampenda na ni mchezaji mzuri,” alisema Kajula na kuongeza;

“Kwa upande wa Saido, tutakuwa naye hadi mwisho wa msimu ndio mkataba wake unamalizika, wengi wanafahamu mkataba wa Saido umemalizika, lakini sio kweli. Kwa ishu ya Chama imekamilika na itawekwa hadharani muda wowote kuanzia sasa, kwamba nini kimeamuliwa ila bado ni mchezaji wetu maana bado ana mkataba na Simba.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live