Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ishu ya Kitayosce kuibeba Pamba?

Pamba FC Ligi Ishu ya Kitayosce kuibeba Pamba?

Sat, 13 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mara Paap! Ni Pamba na JKT Tanzania Ligi Kuu Bara msimu ujao. Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), inasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa mpira wa miguu Tanzania kuona itaamua nini kuhusu timu ya Kitayosce ya Tabora.

Hiyo ni baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwahukumu viongozi wake wawili, Yusuph Kitumbo na Ulimboka Mwakingwe kwa kosa la njama za upangaji matokeo. Kwa karata zilivyo kama likitokea lakutokea Pamba ikishindia pia na mchezo wao wa leo lolote linaweza kuwakuta.

Licha ya kanuni za Ligi ya Championship kuonekana zinaibana Kitayosce, kamati ya maadili iliishia kuwafungia Kitumbo na Ulimboka tu pasipo kuigusa timu hiyo ya Tabora, jambo lililotafsiriwa na wengi kuwa haikutoa adhabu ipasayo kulingana na kanuni ya ligi.

UNDANI WA SAKATA

Aprili mwishoni mwaka huu, klabu ya Fountain Gate inayoshiriki Ligi ya Championship iliibua tuhuma kuwa Kitumbo ambaye ambaye ni mwenyekiti wa TAREFA na timu ya Kitayosce pamoja na Mwakingwe walifanya mbinu chafu za kuwashawishi baadhi ya wachezaji wao kupanga matokeo kwa kuwatumia fedha.

Lengo la mpango huo lilikuwa ni kuwashawishi wachezaji hao wa Fountain Gate waiachie Kitayosce ipata ushindi katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 28. Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Fountain Gate iliwasilisha ushahidi wa jumbe za simu zinazoonyesha miamala ya fedha iliyotumwa kwa baadhi ya wachezaji wake pamoja na sauti za wahusika wakiwashawishi wachezaji wao.

Mara baada ya kuibuliwa kwa tuhuma hizo, kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi, Mei 4 ilitoa taarifa ya kuliacha suala hilo kwa TFF ili ilishughulikie.

"Ikiwa mchezaji au kiongozi atajishughulisha katika kushawishi upangaji matokeo kama ilivyo katika kanuni ya 33(1.1), klabu au mkoa ambao mchezaji au kiongozi anatoka utapigwa faini. Katika makosa mazito itaadhibiwa kwa kuondolewa kwenye ligi, kushushwa daraja, kupunguziwa pointi na kurudisha zawadi," inafafanua kanuni hiyo.

Hata hivyo, kamati ya maadili kwa mujibu wa katiba ya TFF, haina mamlaka ya kushughulikia masuala yanayohusu mchezo na badala yake yenye mamlaka hayo ni ile ya uendeshaji na usimamizi wa ligi.

"Kamati ya maadili inaongozwa na kanuni za maadili za TFF ambazo zitatumika kushughulikia masuala yote yanayoharibu hadhi na maadili ya soka. Kanuni hizi zinazingatia zaidi miiko ya jumla ndani ya mpira wa miguu ambayo yana mahusiano machache au hayana na matukio ya ndani ya uwanja,"inafafanua ibara 44 ya katiba ya TFF.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi, kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi ndio yenye mamlaka ya mwisho juu ya uamuzi wowote unaohusu masuala ya kimchezo kwenye Ligi Kuu, Ligi ya Championship na ile ya First League.

MASWALI TATA

Nini kitafuata baada ya kamati ya maadili kuwaadhibu Yusuph Kitumbo na Ulimboka Mwakingwe? Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi itaishusha Daraja Kitayosce au adhabu itabakia kwa wahusika hao wawili tu?

Kama Kitayosce haitoguswa na adhabu, njama za upangaji wa matokeo zilizofanywa na watiwa hatiani zililenga kunufaisha timu gani wakati mmoja wa wahusika ni mwenyekiti wa timu lakini pia ni mwenyekiti wa chama cha soka cha mkoa husika ambao timu husika inatoka?

Kwa kamati ya maadili kuwahi kutoa uamuzi juu ya sakata hilo, haiwezi kuathiri mwenendo wa uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo kwa sasa inaendelea kushughulikia tuhuma hizo?

Ni muda mrefu sasa Ligi ya Championship imekuwa ikilalamikiwa kutawaliwa na vitendo vya rushwa, upangaji matokeo na hujuma kwa timu na wachezaji, TFF na Bodi ya Ligi ni lini watachukua hatua stahiki za kufuatilia na kukomesha vitendo hivyo badala ya kusubiri hadi timu zijitafutie ushahidi zenyewe?

KUMBUKUMBU ISIYOVUTIA

Hii ni mara ya pili kwa Kitumbo kukutana na rungu la TFF kutokana na makosa ya rushwa na upangaji wa matokeo ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2016 alipofungiwa na kamati ya nidhamu ya TFF kujihusisha na soka maisha baada ya kubainika kujihusisha na upangaji wa matokeo.

Kitumbo akishirikiana na aliyekuwa katibu wa chama cha mpira wa miguu Tabora (Tarefa), Fateh Remtullah walidaiwa kuhusika katika kupanga matokeo ya mchezo wa iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza ambao timu ya Polisi Tabora iliibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro.

Naye Ulimboka Mwakingwe, mwaka 2010 aliwahi kutuhumiwa kutaka kumpa rushwa Shaban Kado aliyekuwa kipa wa Mtibwa Sugar ili aiachie Simba katika mchezo baina ya timu hizo lakini hata hivyo hakuchukuliwa hatua yoyote na vyombo vya kimamlaka.

KWANINI MTU SIYO TIMU?

Eliud Mvela ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Sheria, Hadhi za wachezaji ya TFF alizungumzia hukumu hiyo kuwa;

"Kwanza tunapaswa kuheshimu maamuzi ya kamati hiyo, pia tujiulize kwanini ni hawa hawa watu ambao wamewahi kuhusishwa na mambo kama hayo miaka ya nyuma, ujue hapo kuna shida.

"Kamati imetoa hukumu kwasababu imeshughulikia jambo la mtu mmoja na sio timu, na inadaiwa walifanya jaribio la kupanga matokeo lakini hawakufanikiwa kwasababu wachezaji wa Fountain Gate walitoa taarifa, hivyo mpango huo haukuathiri matokeo ya mchezo pengine ndio maana timu haijapewa adhabu.

"Na hakuna sehemu ambayo kamati imesema pengine kulikuwepo na kikao cha Kamati ya Utendaji ya Kitayosce kilijadili juu ya upangaji matokeo ndio maana amehukumiwa Kitumbo pekee, hivyo kwa kamati hii waliojaribu ndiyo wanaopaswa kuhukumiwa na sio timu," alisema na kuongeza;

"Hata kama mechi ingemalizika ndipo wabaini kuwa kulikwepo na upangaji matokeo lakini kwa mujibu wa Kamati hii ingemwadhibu mtu ndipo adhabu zingine zingefuata kwa wale walioonekana kunufaika na hiyo rushwa."

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya TFF, Elius Mwanjala alipoulizwa na Mwanaspoti juu ya sakata hilo alisema; "Kamati ya Maadili inashughulikia mambo yote ya kimaadili ya viongozi na siyo timu, hivyo kama kutakuwa na masuala ya timu ni kamati nyingine inayopaswa kushughulikia."

PAMBA YACHEKELEA KWAPANI?

Kwa kilichowakuta viongozi wa Kitayosce ni kama Pamba ya Mwanza wanachekelea kwapani kwani kwa mbaali lolote linaweza kutokea wakacheza Ligi Kuu msimu ujao. Pamba yenye pointi 56, iko nafasi ya tatu kama itashinda mechi yao ya leo na Kitayosce kukumbwa na adhabu ya kushushwa,wao wataungana na JKT kwenda Ligi Kuu.

Lakini hilo ni kama kamati itaona kikanuni kuna haja ya kwenda mbali zaidi kuzishughulikia timu husika badala ya kuishia kwa watendaji ambao ni Ulimboka na Kitumbo.

Nini maoni yako kuhusu sakata hili?

Chanzo: Mwanaspoti