Klabu ya Simba inatarajiwa kufanya Mkutano Mkuu wa Mwaka, Januari 21 mwakani, huku ikiwaita wanachama wa klabu hiyo kutoa mapendekezo kwa ajili ya marekebisho ya katiba kama agizo la Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ilivyoitaka ili mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji utekelezeke.
Marekebisho ya katiba ya Simba ni moja ya ajenga ya mkutano huo na kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa juzi na uongozi umewaomba wanachama kujitokeza kwa wingi kutoa mapendekezo yao katika ofisi za sekretarieti au kupita njia ya barua pepe mapema kabla ya Desemba 30.
Katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa na maagizo ya BMT, uongozi wa Simba umeunda Kamati Maalumu ya kuendesha mchakato huo yenye jumla ya wajumbe saba wakiongozwa na Mwenyekiti, Wakili Hussein Kitta akisaidiwa na makamu wake, Wakili Aziza Omary Msangi.
Wajumbe wengine wa kamati huyo ni; Ustaadh Masoud, Zulfika Chandoo, Wakili Moses Kaluwa, Hamis Mkomwa na Mohammed Soloka.
Ajenda za mkutano mkuu huo wa mwaka wa Simba kwa kujibu wa taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi umeanishwa kwenye Ibara ya 22 ya katiba ya Simba ya mwaka 2018 ambayo inajumuisha vipengele 11.
Simba ipo kwenye mchakato wa kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ili uwe wa hisa ambapo wanachama watakuwa na asilimia 51 na asilimia 49 zitakuwa ni za mwekezaji ambaye kwa sasa anatambulika Mohammed ‘Mo’ Dewji.
Hata hivyo, inaelezwa dosari zilizopo kwenye katiba ya sasa toleo la mwaka 2018 linalotoa nguvu kubwa kwa mwekezaji na timu yake kuwa na nguvu kubwa kuliko uongozi wa wanachama unaoongozwa na mwenyekiti wa klabu hiyo.
Hili limekwamisha utekelezaji wa mabadiliko hayo baada ya BMT kutaka ifanyiwe kwanza marekebisho kabla ya mengine kuendelea.