Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ishu ya Dube imejaa ukakasi hadi basi!

Prince Dube 1 Prince Dube

Sun, 10 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa takriban wiki nzima kwenye soka nchini stori kubwa ilikuwa ni sakata la nyota wa Azam FC, Prince Dube aliyeondoka klabuni hapo, akitaka kwenda kutafuta changamoto kwengine. Inafikirisha. Dube kuondoka kwenye timu ambayo mastaa wengi nchini wanaamini ina kila kitu kinachomwezesha mchezaji kukua kisoka. Ndiyo timu namba moja nchini kwa uwekezaji mkubwa na moja ya timu tajiri Ukanda wa Afrika Mashariki.

Dube kaandika barua akiomba aondolewe katika usajili wa timu hiyo inayomiliki uwanja wa kisasa kuliko klabu yoyote hapa nchini na si hilo tu, kasikika katika 'clip' moja inayotembea mitandaoni akidai viongozi wa timu hiyo eti wamegawanyika miongoni mwao kukiwa na mashabiki wa Simba na wale wa Yanga.

Kimsingi, sakata la Dube limekuja ghafla sana. Limekuja katikati ya msimu wa mashindano ya Ligi Kuu Bara na takriban mwezi mmoja na wiki kama mbili tangu dirisha dogo la usajili lilipofungwa. Hapa ndipo panapoacha maswali mengine. Nitaeleza huko chini.

Hata hivyo, lililo wazi na dhahiri ni Dube sio mchezaji wa timu hiyo tena na hata uongozi umeshathibitisha iko hivyo, kwani mchezaji mwenyewe kashasema haitaki timu hiyo, suala ambalo viongozi wamekubaliana nalo.

Kinachosubiriwa kwa sasa ni pande hizo mbili kuachana vizuri kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wao.

Tukiachana na hilo, ukakasi katika ishu ya Dube upo katika mambo mengi. Kwanza, Dube anadai kinachomkwaza Azam FC ni kuwapo kwa makundi ya viongozi ambao wanashabikia timu zingine zinazoshindana na timu hiyo katika Ligi Kuu na hapa ni wazi anazisema Simba na Yanga.

Ni kweli. Inawezekana kuna viongozi wanaoshabikia timu hizo na mashabiki kindakindaki, lakini haiondoi ukweli timu yao inashindania ubingwa wa nchi na timu hizo. Na kama Dube anamaanisha viongozi hao ni mashabiki wa timu hizo hilo halikwepeki, kwani nchi hii unaweza kushabikia timu nyingine lakini ukabaki kuwa na mapenzi na ama Simba au Yanga.

Hivyo Dube hapa ni kama kalazimisha kuweka wazi kilicho wazi. Pengine uzito wa hoja ya Dube dhidi ya viongozi wa Azam FC ungeangukia katika suala la mapenzi yaliyopitiliza dhidi ya Yanga au Simba kiasi cha kusahau wana jukumu la kuhakikisha timu yao inapaswa kusimamiwa na kutekelezewa mahitaji yake na zaidi kama wanaihujumu timu ili Simba na Yanga ziendelee kushinda mechi zake dhidi ya timu yao.

Labda tu nimkumbushe Dube, Simba na Yanga ziko katika mioyo ya karibu asilimia 90 kama sio 100 ya mashabiki wa soka Tanzania kutokana na historia za klabu hizo. Ni vyema katika hili pia akafahamu, hata mmiliki wa Azam FC amewahi kuwa kiongozi mkubwa katika mojawapo wa klabu hizi mbili.

Si hivyo tu, duniani kote klabu zenye nasaba na mashabiki wengi ni zile zilizotengeneza rekodi na historia ya mafanikio kwa miaka mingi. Si ajabu Barcelona na Real Madrid huwezi kuziweka kando katika muktadha wa aina hii katika soka la Hispania kama ilivyo kwa Manchester, Liverpool na Arsenal kule England au Monaco, Lyon na Maseille kwa Ufaransa.

Hizo ni timu ambazo zina mashabiki wengi na zimesomba mpaka mashabiki wanaoshabikia na kujazana katika mechi za mitaani kwao au hata zile za timu zingine.

Ndiyo maana hoja ya Dube katika muktadha huu inapwaya na inakosa mashiko.

Hata hivyo, hivi kama huo ndio ukweli na ni miongoni mwa vitu vilivyokuwa vinamkera, inakuwaje aombe kuondoka sasa? Hivi tangu alipotua Azam mwaka 2020 hivi sasa ndio kagundua hili lipo? Inafikirisha. Pengine Dube ana jambo lake moyoni ambalo anataka kulifanya.

Kwa upande mwingine Dube anafikirisha kuondoka klabuni hapo katikati ya msimu ikiwa ni siku chache tu tangu dirisha dogo la usajili lilipofungwa. Kimsingi, Dube kaikwaza kwa kiasi kikubwa timu hiyo kuondoka sasa wakati ambao haiwezi kusajili mbadala wake.

Kaikwaza zaidi kwa sababu kalazimisha kusepa wakati ikiwa katika kilele cha kupambania rekodi yake ya pili ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa miongoni mwa askari walioaminiwa na uongozi kushinda vita. Hapa napo inafikirisha. Inafikirisha zaidi inapojadilika kama hujuma dhidi ya klabu hiyo.

Nafahamu wapo wachezaji wamewahi kupambania kuondoka katika klabu zao, lakini sina uhakika kama wapo waliofanya hivyo katika mazingira kama aliyofanya Dube yaani mtu anataka kuondoka klabuni mara tu baada ya dirisha kufungwa.

Ndio! Wapo waoshinikiza kuondoka, lakini ilikuwa ni kuelekea dirisha kufunguliwa kama alivyofanya Feisal Salum 'Fei Toto' aliyefanya hivyo wakati wa dirisha dogo la usajili la msimu uliopita, japo alikomaa hata baada ya kufunguliwa na mpaka lilipofungwa.

Huyu alionyesha kutaka kuondoka wakati muafaka ili timu yake kama inataka kusajili ifanye hivyo kuziba pengo lake. Hata Ulaya wapo waliofanya hivyo, lakini sio baada tu ya dirisha kufungwa.

Swali jingine la kujiuliza kuhusu Dube, je anapoondoka katikati ya msimu anakwenda wapi? Atasajiliwa na timu gani wakati kavunja mkataba? Shirikisho la Soka Dunia (Fifa) halina kipengele katika kanuni zake kinachomtetea mchezaji wa aina hii ili asajiliwe na timu nyingine katikati ya msimu.

Ndiyo maana Dube anatuachia maswali. Anakwenda wapi? Kufanya nini? Na kama ameamua kupumzika soka mpaka msimu ujao, ana uhakika na utimamu (ufiti) wake utakuwaje katika timu itakayomsajili dirisha lijalo? Je hataishia kusugua benchi? Yapo mambo yanafikirisha.

Kwa upande wa Azam FC, kuna jambo la kujifunza. Bahati mbaya sana katika soka inaelezwa timu nyingi huwa hazijifunzi kutokana na makosa au changamoto kuanzia ndani ya uwanja hadi uongozini, kwani kilichotokea kwa Dube kinaweza kuletwa na mchezaji mwingine na ikawa hivi hivi.

Kwa wengi Azam FC inaaminika ni timu yenye mifumo bora hususan miundombinu ya uendeshaji na ukuzaji soka ikiwa na kituo bora cha vijana kuliko timu yoyote ya Ligi Kuu Bara, hivyo inapaswa kulinda hadhi yake bila kuruhusu kuathiriwa na mambo yanayokwaza baadhi ya watu - kama anavyodai Dube kukwazika na ushabiki wa timu zingine shindani kupita kiasi.

Inawezekana viongozi wakawa na mapenzi yao kwa Simba au yanga, lakini kuyaonyesha hadharani na kwa uwazi ni tatizo. Hili halipaswi kuonekana. Ni vyema likabakia kuwa ndani ya mioyo yao, wakiamini kuendesha kwao timu kubwa kama hiyo ni tunu waliyo nayo na wanapaswa kuilinda.

Dube anaondoka, lakini anakwenda na picha gani dhidi ya viongozi anaodai ni mashabiki wa timu zingine ilhali wana timu wanayoiongoza? Kumbuka huyu sio Mtanzania. Hili nalo linafikirisha. Yapo mengi yanayofikirisha, lakini kwa sasa tusubiri wamalizane, huenda tukafikirishwa zaidi na zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti