Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ipo siku ‘ndoa’ ya Chama na Yanga itafungwa tu

Chama Vs Jwaneng.jpeg Kiungo wa Simba, Clatous Chama

Sat, 18 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Huwa nasema na nitaendelea kuamini hivyo kila siku. Clatous Chama ndiye mchezaji wa kisasa aliyeweka kiwango cha ubora kwenye Ligi ya Tanzania Bara.

Ni kweli kwa sasa Chama ameshuka. Ni kweli hayupo kwenye ubora aliokuwa nao miaka mitatu iliyopita, ila bado anabaki kuwa kipimo cha mchezaji bora yeyote anayekuja nchini.

Ipo hivi. Ili watu wa soka waweze kusema kama wewe ni mchezaji bora kiasi gani lazima wakufananishe na Chama. Lazima uwe mzuri kama Chama au zaidi ya Chama.

Ndiyo sababu aliposajiliwa Stephane Aziz Ki kwenye kikosi cha Yanga alianza kufananishwa na Chama. Watu walioamini kuwa Aziz Ki ni mzuri kuliko Chama. Wapo walioamini ni mzuri kama Chama. Na wapo wanaoamini bado hajafika kwenye makali ya Chama yule ambaye aliuzwa kwenda RS Berkane.

Kila mtu atabaki na Imani yake lakini hapa hoja yangu ni kwamba ili uwe bora lazima ufananishwe na Chama. Kwanini? Kwasababu Chama alipokuwa kwenye ubora wake alikuwa ndiye mchezaji bora Zaidi wa zama hizi kuwahi kucheza Bongo.

Chama alileta vitu ambavyo hatukuzuea kuviona katika Ligi yetu. Ana utulivu mkubwa sana katika eneo la mwisho. Anatoa pasi za mwisho zilizonyooka. Anajua kufunga. Ameamua mechi nyingi za Simba za kimataifa ambazo zilionekana ngumu. Ndiyo sababu tunasema Chama ni mmoja tu.

Aliposajiliwa Pacome Zouzoua alianza kufananishwa na Chama. Wapo wanaomini kuwa Pacome ni mzuri kuliko Chama. Ila ukweli ndiyo hivyo ili uonekane bora lazima ufananishwe na Chama.

Chama aliufanya mpira uonekane kazi rahisi. Sehemu ambayo wachezaji wengi wangekuwa na papara yeye alitulia na kufanya jambo la kuwashangaza wengi.

Utulivu na akili hii ya Chama ndiyo imeendelea kuwapa Yanga matamanio ya kumsajili hata kwa msimu mmoja. Kila msimu kumekuwa na tetesi kuwa huenda Chama akajiunga na Yanga. Unadhani wanaongopa? Hapana. Yanga ni kweli wanatamani kuwa na Chama siku moja.

Ni kama vile ilivyokuwa hadithi ya Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ wakati akiwa Azam FC. Maneno yalikuwa ni mengi kuwa Sure Boy anacheza Azam FC. Yalisema maneno mengi kuwa yupo Azam lakini moyo wake ulikuwa unaiwaza Yanga. Nini kilitokea baadaye? Alikwenda Yanga.

Ni kama ilivyokuwa ikizungumzwa kwa Haruna Niyonzima wakati ule akiwa Yanga. Kulikuwa na maneno kuwa huenda akatua Simba siku moja. Ni kweli Simba walikuwa wanamtamani lakini hawakuwa na uwezo wa kumnunua kutokana na nguvu ya fedha za Yusuf Manji kwa wakati ule.

Maisha ya Yanga yalivyoyumba kidogo ni kweli Niyonzima alikwenda Simba. Ndiyo soka lilivyo. Kuna wachezaji wanakuwepo timu Fulani lakini kunakuwa na hisia kuwa huenda akajiunga na timu nyingine.

Ndiyo ilivyo kwa Kylian Mbappe ambaye kulikua na hadithi nyingi kuwa siku moja atakwenda Real Madrid. Na sasa Mbappe ameaga PSG na huenda msimu ujao akacheza Madrid.

Ndiyo sababu naendelea kuamini kuwa huenda Chama akacheza Yanga siku moja. Kuna sababu nyingi za kuamini hivyo.

Sababu ya kwanza ni hii ya baadhi ya mashabiki wa Simba kukubali kuwa kama Simba inatakiwa kusonga mbele ni lazima ikubali kuwa mwisho wa Chama utafika. Wamekubali timu yao imruhusu akatafute maisha sehemu nyingine. Viongozi watakubali? Ni jambo la kusubiri na kuona.

Pili, Simba kwa sasa haiwezi kumpa Chama fedha nyingi tena kama walivyokuwa wakimpatia miaka michache iliyopita. Watu wa Simba wanaona kama mchango wake umeshuka ndani ya timu. Hivyo hata kama Simba watampa Chama mkataba mpya, hawatampa wa fedha nyingi. Atakubali kusaini kwa fedha kidogo? Ni ngumu.

Mwisho wa siku Chama anafahamu kuwa fedha yake kubwa ya mwisho ambayo anaweza kuipata nchini ni kuhama kutoka Simba kwenda Yanga. Ni kweli, Yanga wanaweza kumpa fedha nyingi kuliko ambayo anaweza kuipata akiwa Simba. Hii inanifanya niamini kuwa huenda Chama akafanya maamuzi magumu.

Yote kwa yote Yanga nao wamekuwa na matamanio ya kuwa na Chama kwenye kikosi chake siku moja. Ni kweli wana Pacome na Aziz Ki lakini bado wanaona kuna nafasi ya Chama. Ni kweli kabisa. Kiufundi Chama anaweza kuongeza kitu kwenye kikosi cha Yanga.

Kila mtu aendelee kubaki na kile anachokiamini, lakini Imani yangu ni kuwa huenda Chama akacheza Yanga siku moja. Na siku yenyewe haipo mbali.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: