Meneja wa Inter Milan, Simone Inzaghi, amekiri timu yake haitakuwa tishio kubwa katika Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City, baada ya kukamilisha ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya AC Milan kwenye mchezo wa Nusu Fainali uliochezwa juzi jumanne (Mei 16).
Bao la Lautaro Martinez dakika ya 74 kwenye Uwanja wa San Siro liliifanya Inter Milan kuwashinda wapinzani wao wa jiji moja kufuatia ushindi wa magoli 2-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa juma lililopita.
Inzaghi amesema baada ya kuwatambua wapinzani wao katika hatua ya Fainali, hana budi kujiandaa kikamilifu licha ya kufahamu wadau wengi wa Soka duniani wanaiona Inter Milan kama timu ndogo mbele ya Man City.
Amesema Inter Milan ina mipango mikubwa msimu huu, na moja na mpango wao ni kuhakikisha wanamaliza msimu wakiwa mabingwa wa Barani Ulaya, na tayari wameshafika Fainali ya michuano hiyo.
“Ni kawaida unapoenda kukutana na Man City unaonekana ni mdogo, lakini soka huwa wazi, tutapambana kwa sababu dhamira yetu ni kutwaa ubingwa wa Ulaya msimu huu, ni lengo letu kubwa sana ambalo tunapaswa kulitimiza.”
“Tunafahamu Man City wana kikosi bora na imara, na ndio maana kimefanikiwa kuitoa Real Madrid ambayo pia ilitazamwa kwa ukubwa kabla ya mchezo wa jana.” amesema Inzaghi
“Nimetazama mechi yao, nimejifunza vitu vingi sana ambavyo vitanisaidia katika maandalizi ya kuelekea mpambano wa Fainali.”
Man City iliiduwaza Real Madrid jana Jumatano (Mei 17) kwa kuichapa 4-0 katika Uwanja wa Etihad mjini Manchester, huku timu hizi zikitoka sare ya 1-1 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa mjini Madrid.