Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Inter Milan yaitibulia Arsenal kwa Lautaro Martinez

Lautaro Martinez Mahakama Lautaro Martinez

Tue, 18 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Rais wa Inter Milan, Giuseppe Marotta ameweka wazi kwamba wameshafikia makubaliano na straika wao Lautaro Martinez na wanatarajia kukamilisha mchakato wa kumsainisha mkataba mpya katika siku chache zijazo.

Ikiwa fundi huyu kweli atasaini, basi litakuwa ni pigo kubwa kwa Arsenal iliyokuwa inatajwa kutaka kumsajili katika dirisha hili ikiwa ni moja ya mapendekezo ya kocha wao Mikel Arteta.

Lautaro ambaye msimu uliomalizika alikuwa mfungaji bora wa Serie A, na kuiwezesha Inter Milan kuchukua ubingwa wa ligi hiyo, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.

Staa huyu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 26, hivi karibuni alipoulizwa juu ya hatma yake kwenye kikosi cha Inter alieleza kwamba bado ana mkataba, hivyo kuondoka ama kubaki wataamua mabosi wa timu hiyo na sio yeye.

Staa huyo amekuwa katika mafanikio na alishinda Kombe la Dunia 2022 akiwa na kikosi cha Argentina katika fainali zilizofanyika huko Qatar.

WAWAKILISHI wa beki wa pembeni wa Chelsea, Ian Maatsen, 22, wametua jijini Birmingham kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mabosi wa Aston Villa ili kujadili dili la beki huyo kutua Villa Park katika dirisha hili. Maatsen amevutia timu nyingi Ulaya kutokana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita alipokuwa akicheza kwa mkopo Borussia Dortmund ambayo ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa na kupoteza mbele ya Real Madrid.

IPSWICH, Southampton, Leicester na Leeds ni kati ya timu zinazohitaji huduma ya beki wa Tottenham na Wales, Joe Radon, 26, katika dirisha hili.

Radon hajapata nafasi kubwa ya kucheza kwa msimu uliopita na hiyo ndio imesababisha awasilishe barua ya kuomba kuondoka kwa mkopo au auzwe jumla kwa ajili ya kwenda timu itakayompa nafasi kubwa ya kucheza ili kulinda kipaji chake.

TOTTENHAM imetuma baadhi ya maofisa wake kwenda Italia kufanya mazungumzo na Bologna ili kumsajili beki wa timu hiyo na Italia, Riccardo Calafiori katika dirisha hili.

Calafiori, 22, alikuwa chachu ya kufanya vizuri kwa Bologna kwa msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Italia.

Mazungumzo baina ya maofisa hao wa Spurs na Bologna yanadaiwa kwenda vizuri ila mwafaka haujafikiwa.

ASTON Villa na Juventus zinadaiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kukamilisha dili la Douglas Luiz kutua Juve huku McKennie na Iling-Junior wakienda Villa kama sehemu ya mabadilishano. Mbali ya Luiz kutua Juventus, pia taarifa za wikiendi iliyopita zimefichua kwamba mchumba wake anayecheza Villa ya wanawake Alisha Lehmann naye yupo kwenye mazungumzo ya kutua timu yao ya wanawake Italia.

ROMA inafikiria kumsajili beki wa Borussia Dortmund, Mats Hummels, 35, katika dirisha hili baada ya staa huyo kutangazwa kwamba ataondoka bure mwisho wa msimu huu.

Hummels ambaye ni mmoja kati ya mastaa waliocheza kwa kiwango bora muda wote aliohudumu ndani ya kikosi hiki cha Dortmund amekuwa akihusishwa pia na baadhi ya timu za Marekani.

NEWCASTLE imeanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili winga wa Chelsea, Noni Madueke, 22, katika dirisha hili ili kuboresha zaidi eneo lao la la ushambuliaji lililokuwa na upungufu kwa msimu uliopita.

Mabosi wa Newcastle wanataka kuipata huduma ya Noni aidha kwa mkopo au kumnunua jumla, ingawa kipaumbele chao cha kwanza ni kumnunua.

NEWCASTLE inatarajiwa kutuma ofa nyingine mpya kwa ajili ya kuipata saini ya kipa wa Burnley, James Trafford, 21, katika dirisha hili baada ya ofa yao ya kwanza ya Pauni 16 milioni kukataliwa. Mabosi wa Newcastle walivutiwa na kiwango cha Trafford licha ya kuwa mmoja kati ya makipa waliofanya vibaya kwenye Ligi Kuu England msimu uliomalizika.

Chanzo: Mwanaspoti