Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Inshu ya Kakolanya kumbe siriasi

Kakolanya Yt.jpeg Beno Kakolanya

Fri, 28 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Leo Ijumaa, Simba itakuwa Uwanja wa Mohammed V, nchini Morocco kuanzia saa 4:00 usiku ikicheza mechi ya mkondo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC huku kukiwa na sapraizi kwenye ukuta.

Kipa mzoefu ambaye hajadaka sikunyingi, Beno Kakolanya ataanza akichukua nafasi ya Ally Salim ambaye ameonyesha umahiri mkubwa kwenye siku za karibuni.

Awali, benchi la Ufundi la Simba liliwasapraizi mashabiki kwa kumuanzisha kinda Salim kwenye mechi tatu zilizopita dhidi ya Ihefu (2-0), Yanga (2-0) na Wydad (1-0) huku Beno akikaa benchi na Aishi Manula jukwaani kutokana na majeraha.

Lakini huenda leo akadaka Beno ambaye anahusishwa na kujiunga na Singida Big Stars msimu ujao, kubwa zaidi ikielezwa ni uwezo wake wa kujiamini ambao utaweza kumudu presha ya mashabiki wa Wydad ambao si rafiki kwa timu pinzani haswa mlinda mlango.

Mashabiki wa Wydad maarufu kama 'Ultas Avanti' wamekuwa wakikaa nyuma ya lango la mpinzani na kumbugudhi kipa kwa kelele na presha jambo lililowastua Simba na kuanza mipango ya kumrejesha Beno langoni, hapo kesho.

"Uzoefu wake ni muhimu kukabiliana na presha ile,Beno amezoea mambo haya," alidokeza mmoja wa viongozi Simba.

Kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho', ndiye ameachiwa jukumu la kuamua ampange nani leo na anafahamu changamoto ya nchini humo.

Simba inahitaji ushindi au sare kwenye mechi ya leo ili kutinga nusu fainali baada ya kushinda mechi ya kwanza kwa bao 1-0, lililofungwa na Straika Mkongomani, Jean Baleke Jumamosi iliyopita Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Chanzo: Mwanaspoti