Kuelekea kwenye michuano ya kimataifa, uongozi wa Simba umeanza kusaka beki wa kati atakayeweza kuja kuwa mbadala wa Henock Inonga ambaye ana majeraha.
Inonga atakuwa nje ya kikosi kwa takribani wiki tatu baada ya kuumia bega kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate na tayari amerejea kwao DR Congo kujiuguza.
Chanzo chetu kutoka Simba kimesema kuwa, kutokana na uwepo wa michezo mingi ya ligi kabla ya kucheza michuano ya kimataifa, Kocha wa Simba, Oliviera Robertinho ameuomba uongozi huo kufikiria namna ya kuongeza beki wa kati.
“Hadi sasa kocha anaonekana kuwa na wasiwasi wa beki wa kati, jambo ambalo limewafanya viongozi kuanza kufikiria kupata mbadala wa Inonga ili aje kusaidiana na Kennedy Juma na Che Fondoh Malone.
“Tayari wanaendelea kuona kama watapata beki mzawa kabla ya michuano ya kimataifa kuanza kwani hofu ni juu ya majeraha ya Inonga kama yatapona mapema zaidi,” kilisema chanzo hicho.