Kurejea kwa nyota Henock Inonga, Moses Phiri na Peter Banda ambao walikuwa majeruhi, kumempa furaha Kocha Msaidizi wa Simba SC, Juma Mgunda kuelekea mchezo wa Azam Sports Federation dhidi ya Coastal Union.
Mgunda ambaye anakinoa kikosi kuelekea mchezo huo utakaopigwa Januari 28, 2023 katika Dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar, amesema anafarijika kuona nyota hao pamoja na wale ambao walikuwa wakitumikia adhabu za kadi wamerejea.
"Nimefurahi kuwaona nyota wangu waliokuwa majeruhi wamerejea lakini pia waliokuwa na adhabu nao wameingia kikosini bila kusahau wachezaji wapya ambao tumewasajili kwenye dirisha dogo nao wameanza kuingia kwenye mfumo wetu," alisema Mgunda.
Mgunda atasimama kwenye benchi la timu hiyo katika mchezo huo baada ya Kocha Mkuu, Roberto Oliviera 'Robetinho' kuelekea nchini kwao Brazil kwa kile kilichoelezwa kuwa, anakwenda kushughulikia hati ya kusafiria kabla ya kuanza kwa mashindano ya Kimataifa Februari mwaka huu.