Nyota wa Simba SC ambao walikuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha, kesho wanatarajia kurejea dimbani kuwakabili Singida Big Stars katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar.
Akizungumzia mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema wanayo furaha kuona nyota hao ambao walipata majeraha kwa nyakati tofauti pamoja wengine wote waliokuwa na majeruhi, wamerudi kikosini.
"Mchezo wetu wa Singida tunakwenda kucheza nao kwa mara ya kwanza tukiwa tumekamilika kwa kiasi kikubwa tofauti na michezo kadhaa iliyopita ambayo wachezaji wetu walikuwa wakipishanapishana kutokana na majeraha.
"Tunafurahi kuona Peter Banda ambaye aliumia kwenye mchezo wetu wa mzunguko wa kwanza dhidi ya haohao Singida, anarejea kuitumikia Simba sambamba Henock Inonga lakini pia Phiri ambaye naye alikuwa majeruhi, amepona japo anaweza asitumike kwa mchezo wa kesho sababu hajawa na utimamu wa mwili wa asilimia mia lakini mechi zinazofuata tunaamini atacheza," alisema Ahmed.